HALMASHAURI ya Manispaaa ya Iringa imepiga marufuku ujenzi holela unaoendelea katika milima ndani ya mji wa Iringa .
Kauli hiyo imetolewa leo na mstahiki
meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi wakati
akizungumza na wanahabari ofisini kwake.
Alisema kuwa udhaifu wa usimamizi wa sheria katika maeneo mbali mbali ndio umepelekea ujenzi holela kuendelea.
Hata hivyo alisema nyumba ambazo
zinajengwa kiholela katika mji wa Iringa zitaendelea kuvunjwa iwapo
itabainika kuwa zimejengwa kiholela.
Kuhusu uwekezaji alisema kuwa vipo
viwanja kama vitatu ambavyo vinahitaji uwekezaji na hivyo kuwataka
wananchi kujitokeza kuwekeza katika maeneo hayo.
Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Dkt.Fenella Mukangara akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza Jipya la Kiswahili
RAIS KIKWETE AKUTANA WAZIRI WA NISHATI NA MIGODI WA ALGERIA LEO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Januari 7, 2014, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria Mheshimiwa Youcef Yousfi ambaye yuko katika ziara ya siku sita nchini.
Katika ziara hii, Mheshimiwa Yousfi na
ujumbe wake unaojumuisha viongozi wa mashirika ya umma, wanatarajia kutembelea
kituo cha umeme cha Gridi ya Taifa cha Ubungo mjini Dar es Salaam, ujenzi wa
bomba la gesi katika eneo la Vikindu na Mkuranga mkoani Pwani, machimbo ya
Mererani na Minjingu mkoani Manyara.
Rais Kikwete ameeleza kufurahishwa kwake
na ziara hiyo, akisisitiza kwamba Tanzania na Algeria zimekuwa marafiki na
washirikia wa karibu wa siku nyingi katika masuala ya siasa na uchumi, kufuatia
misingi imara iliyowekwa na waasisi wa nchi hizo - Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Mheshimiwa Ahmed Ben Bella,
Rais amebainisha kwamba ushirikiano wa
nchi hizi mbili ni muhimu sana sio tu katika kuendeleza uhusiano wao wa
muda mrefu, bali pia katika uwekezaji na utafutaji na uchimbaji wa
mafuta na gesi pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu.
Alisema Rais: "Tunahitaji washirika wazoefu, waaminifu na wenye ujuzi katika
sekta ya mafuta na gesi kama Algeria katika kuendeleza sekta hiyo ambayo ni
mpya kwetu”.
Alitolea mfano wa uzoefu wa miaka mingi
wa Algeria katika uchimbaji na usafirishaji wa gesi asilia katika mradi wa
bomba la gesi la Maghreb–Europe, unaounganisha machimbo ya gesi ya
Hassi R'Mel nchini Algeria, na kusafirisha gesi asilia hadi nchi za Morocco,
Hispania na Ureno
"Tanzania itanufaika sana na juzi na uzoefu wa
Algeria katika sekta ya gesi hasa katika wakati huu ambapo Shirika la Taifa la Maendeleo
ya Petroli (TPDC) limepewa jukumu la kujiendesha kibiashara hivyo linahitaji
washirika mahiri", alisema Rais
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR
ES SALAAM
07 Januari, 2014
Ndege aliyotumia rais Dr Jakaya Kikwete ikitua uwanja wa ndege nduli Iringa
Msafara wa waziri mkuu Mizengo Pinda ukiwasili uwanja waNdege Nduli Iringa
Mafundi ujenzi wakijenga kaburi la Dr Mgimwa
Barabara iliyetengenezwa kwa ajili ya ugeni wa kitaifa japo eneo hilo la barabara ya Masumbo - Kiponzero lilikuwa korofi siku nyingi
Waziri Mkuu Mizengo Pinda baada ya kuwasili nyumbani kwa Dr Mgimwa kijiji cha Magunga
.......................................................
WAKATI
Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Jakaya Kikwete akiwa katika
mtihani wa kuziba nafasi ya aliyekuwa waziri wa fedha Dr Wiliam
Mgimwa aliyezikwa juzi kijijini kwake Magunga Kalenga wilaya ya Iringa ,
wabunge na mawaziri mbali mbali wameibuka na kumzungumzia Dr Mgimwa
huku mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe akidai kuwa kati ya
mawaziri wasikivu kwa wabunge alikuwa ni Dr Mgimwa na kuwa hakuwa na
ndoto ya kumshambulia ama kumsema vibaya bungeni.
Akiungumza mahojiano maalum na mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com juu ya kifo cha Dr Mgimwa
kilichokuwa kikirushwa moja kwa moja na Radio Nuru Fm iliyopo mkoani
Iringa , Mbunge Filikunjombe alisema kuwa mbali ya kuwa wananchi
wa jimbo la Kalenga wamempoteza mbunge mchapa kazi ila bado Taifa
limempoteza waziri mwadilifu zaidi.
Kwani
alisema kwa kipindi chake chote cha uwaziri alikuwa ni msikivu na
mwenye kupenda kushauriwa na kila mmoja katika kuitumikia nafasi
hiyo na kuwa Dr Mgimwa alikuwa ni tofauti na mawaziri wengine ambao
wameendelea kuikwamisha serikali ya rais Dr Jakaya Kikwete kwa
kutokuwa wasikivu .
Filikunjombe ambae alipata kumshambulia bungeni aliyekuwa waziri wa fedha kabla ya Dr Mgimwa Bw Mustafa
Mkullo kwa kushindwa kutoa fedha kwa wakati kwa ajili ya kununua
mahindi ya wananchi wa Ludewa ,alisema kuwa Dr Mgimwa kwa kila
jambo ambalo alikuwa akielezwa na wabunge alikuwa akiwatekelezea kwa
wakati.
"Binafsi
nimeumia sana na kifo cha Dr Mgimwa kwani katika ndoto zangu za
mbeleni sikufikiria kuja kutofautiana na waziri Dr Mgimwa ... kwani
alikuwa ni mtu wa kujishusha na kutenda na sio kujisikia na kupuuza
mambo"
Filikunjombe alisema pia la kifo chake linaumiza wengi ambao walipata kufanya nae kazi kwa karibu wakiwemo wabunge .
Naibu waziri wa chakula na ushirika Adam
Malima alisema kuwa siku zote Dr Mgimwa alikuwa ni wa mfano
katika utendaji kazi wake na kuwa kati ya viongozi waadilifu katika
Taifa pia alikuwa ni mmoja wapo.
Alisema
Dr Mgimwa alikuwa akiishi maisha ya kawaida sana ukilinganisha na
wengine na kuwa hakupenda kujilimbikizia mali ila alipenda zaidi
kulitumikia Taifa lake kwa nafasi aliyokuwa nayo ya uwaziri na
kuwatumikia wana Kalenga kwa nafasi yake ya ubunge.
Malima
aliwataka watanzania kuendelea kutafakari na kuendelea moyo wa
kulipenda Taifa na kuepuka kauli za kichochezi ambazo hazina maana
katika Taifa letu .
Mbunge
wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa alisema kuwa miongoni
mwa mawaziri wachakapa kazi ambao Taifa limewapoteza ni pamoja na Dr
Mgimwa .
Msigwa
alisema kwa kipindi chote cha uongozi wake Dr Mgimwa hakuwa ni
mwenye kujisikia na alikuwa akisikiliza kwa makini na kukubali
kushauriwa na kamwe hakumpuuza mbunge yeyote wakati wa uchangiaji bungeni juu ya wizara yake.
Hata
hivyo mbunge Msigwa alisema kuwa itikadi za vyama vinapaswa kuwekwa
kando katika kipindi hiki cha maombolezo kwa wana Kalenga na
watanzania na kuwa ni vema kwa kila mmoja kujitafakari yupo upande
gani katika kulitumikia Taifa na kuwa wapo baadhi ya watu wamekaa
sana duniani na badala
ya kulipa Taifa msaada kwa uwepo wao ila wamekuwa ni hasara katika
Taifa na wapo waliishi kwa muda mfupi na wameonyesha mchango wao
mkubwa katika Taifa.
Naibu
Waziri wa Fedha, Janet Zebedayo Mbene
akielezea jinsi alivyopata kufanya kazi na Dr Mgimwa alisema kuwa ni
kiongozi aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji na alikuwa tayari
kuwashauri waliopo chini yake kwa lengo la kuifanya wizara yake
kuendelea kuwa bora zaidi.
Nyumbani kwa Dr Mgimwa kijiji cha Magunga
Mbene
alisema kuwa mbali ya Dr Mgimwa kuwa waziri ila alikuwa
akijichanganya na wafanyakazi wa chini na kuwaelekeza kwa upendo pale
ambao walikuwa wanahitaji msaada wake na kuwa siku zote alikuwa ni
mwenye furaha na mwenye kujishusha zaidi asiyependa makuu katika
wizara yake.
MATOKEO YA SENSA YA TEMBO NCHINI KUTANGAZWA JANUARY 10 JIJINI DAR ES SALAAM
ASAS DAIRY FARM NI DARASA KWA WAFUGAJI TANZANIA
Ndama waliozaliwa siku za hivi karibuniMAAZIMIO YA KIKAO CHA DHARURA CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU HATUA ZA KINIDHAMU DHIDI YA WANACHAMA ZITTO ZUBERI KABWE, DR. KITILA MKUMBO NA SAMSON MWIGAMBA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (katikati), akiwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa (kushoto) na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohamed wakati wa Kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jijini Dar es Salaam
................................................................................
Kamati Kuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilikaa kikao cha dharura ili kupokea,
kujadili na kuamua juu ya utetezi wa mashtaka ya ukiukaji wa Katiba, Kanuni na
Mwongozo wa Chama yaliyokuwa yanawakabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto
Zuberi Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba. Kikao hicho cha dharura
kilifanyika Dar es Salaam kati ya tarehe 3-4 Januari, 2014.
Kabla ya kuanza kwa
kikao, Kamati Kuu ilipokea taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka
dhidi ya CHADEMA katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Aidha,
Kamati Kuu ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda ya
kuizuia Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na kuamua
suala la uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe.
Kutokana na amri hiyo ya Mahakama
Kuu, Kamati Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka dhidi yake.
MASHTAKA
Watuhumiwa wote
watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka 11 yanayohusu ukiukaji wa vifungu mbali
mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama, Kanuni za Kusimamia
Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa Chama na Mwongozo wa Kutangaza
Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka
yote yalitokana na watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko,
2013 kama ifuatavyo:
Endelea.......
Endelea.......
1. Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa
Chama Taifa Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;
2. Kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi
vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa
Ushindi’ nje ya utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa
nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa;
3. Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila
kupitia vikao halali vya Chama;
4. Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini
na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii;
5. Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au
kuzua migogoro ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;
6. Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya
Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa
Mwongozo wa Chama;
7. Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania
uongozi ndani ya Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
8. Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la
kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
9. Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya
majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa Chama;
10.
Kukashifu Chama na
viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge; na
11.
Kuchochea mgawanyiko
ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge.
UTETEZI WA
WATUHUMIWA
Watuhumiwa wote
walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya utetezi huo wa maandishi, Dr. Kitila Mkumbo
na Samson Mwigamba waliitikia wito wa Kamati Kuu wa kujitetea kwa mdomo mbele
yake.
Hata hivyo, siku ya utetezi wao, ni Dr. Kitila Mkumbo peke yake aliyejitokeza
kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Katika utetezi wake wa maandishi,
licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa
Mabadiliko 2013, Dr. Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa Samson Mwigamba –
alikanusha na kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama, Kanuni zake na
Mwongozo wa Chama.
Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha “kila tuhuma
mojamoja na kwa ujumla wake dhidi ya[ke]”, na kwamba mashtaka hayo sio ya kweli
na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa Chama.
Aidha, licha ya
kukiri kwake katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana kwamba
walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara
hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu kwamba “waraka husika ulikuwa ni wa
siri na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha … wanachama au viongozi wa
CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Samson Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa
katika Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa
M2, mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2 lakini hayuko
tayari kumtaja mbele ya Kamati Kuu hadi atakapowasiliana naye!
USHIRIKI WA ZITTO
ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA MABADILIKO
Itakumbukwa kwamba
katika kikao cha Novemba 2013, Dr. Kitila Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe walikataa
kata kata kuhusika kwa Zitto Zuberi Kabwe katika maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko.
Aidha, Zitto Zuberi Kabwe alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia
Mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara
nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi.
Hata hivyo, wakati wa
mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila Mkumbo alikiri kwamba yeye na
waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi Kabwe briefing juu ya Mkakati
na kwamba alikuwa anaufahamu. Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya
baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA
Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati
Kuu ya Novemba iliyowavua madaraka.
Zaidi ya hayo, baada
ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu ya mabadiliko ya Katiba ya Chama uliotumwa na
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama wakati huo Shaibu Akwilombe Julai 2006
unaothibitisha kwamba mabadiliko ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi
yalifanywa kwa uwazi na kwa kushirikisha ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo
alikataa kata kata kujadili suala hilo kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko
yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Kuhusu tuhuma zao
kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Chama unaofanywa na Mwenyekiti wa
Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha Anthony Komu na kwamba taarifa za
matumizi ya fedha ni siri ya viongozi hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa
mbali mbali za fedha zilizowasilishwa mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama
ambavyo yeye mwenyewe na Zitto Zuberi Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati
Kuu.
Aidha, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi
michango ya Mzee Jaffer Sabodo na michango mingine ya watu binafsi
zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake kuwasilishwa kwenye vikao vya
Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi Kabwe.
Zaidi ya hayo, Dr.
Mkumbo alionyeshwa nyaraka za manunuzi ya vifaa vya Chama kama vile vile
pikipiki, kadi, bendera, n.k, na jinsi ambavyo uamuzi wa manunuzi hayo
yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao wenyewe ni wajumbe na walihudhuria vikao
husika.
Vile vile, Dr. Mkumbo alionyeshwa ushahidi wa maandishi kwamba
Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa namna yoyote ile katika manunuzi hayo na
hakuna karatasi yoyote inayoonyesha saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya
vifaa hivyo.
Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba
CHADEMA ina mkataba wowote na watu binafsi wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama
kwa vile Kamati Kuu ya Chama katika vikao ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo
na Zitto Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa
hivyo na kuviuza kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote haya, Dr.
Kitila Mkumbo hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati Kuu.
MAAMUZI YA KAMATI
KUU
Baada ya kusikiliza
utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na baada ya kumhoji kwa kirefu, Kamati Kuu
imeridhika bila mashaka yoyote kwamba Mkakati wa Mabadiliko 2013 haukuwa na
lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa
Chama peke yake.
Mkakati huo ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa
Chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa
kutumia tuhuma za uongo za ufisadi.
Hii ni kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu,
Chama cha siasa ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi
kuaminiwa na wananchi kama tumaini lao la ukombozi.
Kamati Kuu
imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali mbali zilizoandaliwa na Zitto Zuberi
Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake wakitumia vitambulisho bandia katika
mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa kukibomoa Chama
umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu.
Mkakati huo ulihusisha pia hujuma
dhidi ya Chama kwa kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbali mbali kama
ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida
Mjini ambapo Zitto Zuberi Kabwe alishiriki moja kwa moja.
Kwa sababu zote
hizo, Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo:
1.
Kwamba
kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wafukuzwe
uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na
2.
Kwamba,
kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa ya Katiba ya
Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya Chama
visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe,
viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote
walipo katika nchi yetu na nje ya Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa namna
yoyote mikutano yoyote ya nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya
kisiasa itakayofanywa na Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la
CHADEMA.
--------------------------------
Dr. Wilbrod P. Slaa
KATIBU MKUU