Wednesday, January 31, 2018
Rais Dkt. John Magufuli amezindua mpango wa hati ya kusafiria ya kielektroniki ya Tanzania ambayo itarahisisha taratibu za utoaji wa hati, ukusanyaji wa maduhuli, kuimarisha ulinzi na usalama na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ikiwemo mbuga za wanyama.
Akizindua mpango huo Jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amesema suala la uhamiaji ni nyeti na muhimu sana hasa kwa usalama wa nchi ambapo hapo awali hakukuwa na utaratibu makini wa kutoa hati za kusafiria, vibali vya ukaaji na ukusanyaji wa mapato kutoka maombi ya hati za kusafiria.
Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Ireland kwa ufadhili wa Mradi huo ambao umegharimu Shilingi Bilioni 127 huku akiipatia Idara ya Uhamiaji nyumba 103 Mjini Dodoma pamoja na Shilingi Bilioni kumi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za uhamiaji Mjini Dodoma ikiwa ni hatua ya serikali kuhamia Dodoma.
Balozi wa Ireland hapa nchini Paul Sherlock amesema nchi yake ina uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa mifumo ya kilektroniki hivyo itasaidia kutekeleza Mpango wa Hati ya Kusafiria ya Kielektroniki ya Tanzania.
Kamishna Mkuu wa Idara ya Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala amesema mpango huo utarahisisha kuhudumia wageni wengi wanapoingia kwa mkupuo, kudhibiti wahamiaji haramu na kuongeza mapato ambapo katika kipindi cha kutoka Julai hadi Desemba mwaka jana Idara ya Uhamiaji ilikuwa imekusanya Shilingi Bilioni 85 kutokana na maduhuli.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dokta Mwigulu Nchemba amesema utaratibu huo ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa pamoja na kuziba mianya ya kugushi hati za kusafiria kama ilivyokuwa hapo awali.
Thursday, January 11, 2018
Subscribe to:
Posts (Atom)