Mageuzi makubwa usafiri wa Reli yaja
Serikali yatangaza mageuzi usafiri wa reli
Dodoma. Serikali imekamilisha taratibu za
ununuzi wa vichwa vipya 13 vya treni na mabehewa 355 ambayo yataanza
kuwasili nchini kati ya Julai na Desemba mwaka huu.
Serikali inashirikiana na Serikali za Rwanda na
Burundi katika uendelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Dar es
Salaam-Isaka-Musongati kwa kiwango cha kimataifa.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alitoa
kauli hiyo bungeni mjini Dodoma juzi usiku wakati akiwasilisha bajeti ya
wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 inayofikia Sh527 bilioni.
Alisema kazi inayoendelea sasa ni kumtafuta
mshauri (Transact Advisor) atakayekuwa na jukumu la kuandaa, kusimamia
na kuongoza mpango wa kuwapata wawekezaji watakaojenga reli hiyo.
“Kazi ya usanifu wa kina wa kuinua kiwango cha
Reli ya Isaka-Mwanza ilianza Septemba 2013 na inatarajiwa kukamilika
Julai 2014 kwa gharama ya Sh4.53 bilioni...Hatua hizi ni muhimu katika
kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuboresha Reli ya Kati kwa kiwango cha
kimataifa (standard gauge)” alisema Dk Mwakyembe katika hotuba yake
hiyo.”
Pia Dk Mwakyembe alisema kuwa tayari mtaalamu
mwelekezi amepatikana kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu
wa awali wa ujenzi wa Reli ya Mtwara-Songea-Mbambay.
Mkataba wa kutekeleza kazi hiyo itakayohusisha pia
ujenzi wa reli ya mchepuko kwenda Mchuchuma na Liganga utasainiwa
wakati wowote kabla ya mwisho wa Juni mwaka huu.
Pia mshauri mwelekezi, Kampuni ya Cowi kutoka
Denmark ameanza kazi ya usanifu wa uboreshaji wa njia ya Reli ya
Tanga-Arusha na usanifu huo utagharimu Sh5 bilioni.
Katika hatua nyingine, Dk Mwakyembe alisema
Kampuni ya H.P Gauf ya Ujerumani inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu
na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli mpya ya Arusha-Musoma.
Ununuzi wa mabehewa
Dk Mwakyembe alisema katika mwaka ujao wa fedha wa
2014/2015, Serikali imetenga Sh126.9 bilioni kununua vichwa vipya 11
vya treni na mabehewa 204.
Alisema fedha hizo zitatumika pia kufanya matengenezo ya njia ya reli ya kati yenye mtandao wa urefu wa kilometa 2,707.
No comments:
Post a Comment