Friday, October 24, 2025

Ufugaji wa mbuzi nchini Tanzania una fursa nzuri.

Wakulima wadogo wanaoweza kuanza kidogo kidogo kulingana na mazingira yao kwa kutumia rasiliali zilizopo kwenye maeneo yao ikiwemo miti ya kujenga mabanda, majani yanayopatikana kulishia mifugo, madawa ya asili kutibu mifugo yao, wanafamili waliopo kuchunga na kusimamia mbuzi wako na rasilimali nyingine ikiwemo miti, mchanga,maji , mabaki ya vyakula n.k.. Lakini mafanikio makubwa yanahitaji usimamizi mzuri, uchangamfu wa soko na kuwekeza katika kuwapatia mbuzi wako lishe nzuri ili wapate afya na uzalishaji uongezeke. Mfano unaweza kukua sana kibiashara  ikiwa utaelewa soko lako, aina ya mbuzi unaofuga na kutunza kumbukumbu za gharama zako ili ujue wapi pana kugharimu zaidi ili utafute mbinu za kupunguza gharama.

Ni vizuri uwe na mpango wa biashara (business plan) ya ufugaji wa mbuzi unapoanza kwa mfano unaanza na mbuzi 20–50, ili kujipanga kujua unatoka wapi, unaelekea wapi na uendeje ufike unapotarajia


Picha kwa hisani ya Biosciences, imeandaliwa na Emmanuel Edwin Minja #ShambaniUpdates # #ShambaniNews #ItawatuTanzania

 

Ufugaji wa mbuzi ni fursa inayolipa


 Kuna soko kubwa na la kudumu

Mbuzi wanahitajika kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi na hata mbolea. Mahitaji haya yapo mijini na vijijini mwaka mzima hivyo ni fursa.

Uwekezaji wa awali si mkubwa

Ukilinganisha na uwekezaji wa ng’ombe, gharama za kuanzisha ufugaji wa mbuzi ni ndogo (linahitajika banda, chakula, ununuzi wa mbuzi, msimamizi au mchungaji , gharama za matibabu , chanjo n.k).

Wanastahimili mazingira magumu

Mbuzi ni miongoni mwa wanayama wanavumilia ukame na magonjwa fulani, hivyo wanafaa hata maeneo yenye hali ngumu ya hewa.

Wanazaliana kwa haraka

Jike linaweza kuzaa watoto 2–3 mara mbili kwa mwaka ukipata mbegu bora, hivyo kuongeza idadi ya mifugo yako kwa kasi.

Bidhaa nyingi kwa faida : Nyama (chevon) ; Maziwa yenye virutubisho vingi ; Ngozi bora ; Mbolea ya asili nzuri


Misingi, kanuni na taratibu nzuri za ufugaji bora wa mbuzi

1. Uchaguzi wa aina bora ya mbuzi : 

Kwa maziwa: Mbuzi wa SaanenToggenburg au Alpine.

Kwa nyama: Mbuzi wa BoerGalla au Small East African (Mbuzi wa kienyeji walioboreshwa).

2. Makazi (Banda/zizi) Liwe safi, lenye hewa ya kutosha na linalokinga mvua na jua. Kama ni sakafu inashauriwa iwe na mteremko mdogo ili maji na uchafu vitoke kirahisi. Zingatia nafasi ya kutosha kwa kila mbuzi (~1.5 m² kwa mmoja).

3. Lishe bora

  • Wape majani mabichi, mikunde (lucerne, desmodium) na nyasi zilizokaushwa.

  • Ongeza chakula cha ziada (concentrates) kama pumba, dagaa na chumvi ya madini.

  • Hakikisha wana maji safi muda wote.

4. Afya na usafi

  • Chanjo za mara kwa mara dhidi ya magonjwa (kama PPR, CBPP na nimonia).

  • Dhibiti minyoo ya ndani na nje kwa kutumia dawa.

  • Dumisha usafi wa zizi na vyombo vya kulia chakula.

5. Uzalishaji na uongezaji wa thamani

  • Hakikisha unapanga uzalishaji kwa kuchagua madume bora.

  • Fanya usajili na kumbukumbu za uzalishaji (tarehe ya kuzaa uzito, afya).

  • Zingatia kutoa bidhaa zenye ubora (maziwa yaliyopakiwa vizuri, nyama safi, ngozi kavu vizuri n.k).

6. Masoko

  • Unaweza kutafuta mikataba na wauzaji wa nyama, maziwa, mighahawa au hoteli.

  • Shirikiana na vikundi au vyama vya wafugaji ili kupanuka na kuongeza nguvu yako ya soko.

Mfano wa makadirio ya faida 

Mfugaji mwenye mbuzi 20  anaweza kupata kupata faida kwa wastani :

  • Maziwa: lita 2–3 kwa siku × mbuzi 15  × miezi 8 ( Kuna miezi hukamui) = zaidi ya lita 7,000 kwa mwaka.

  • Chukulia bei ya maziwa: Kwa lita Tshs 1,500  ⇒ utapata zaidi ya Tsh 10 milioni kwa mwaka.

  • Utapata uzao wa watoto wa mbuzi: wastani wa 30–40 kwa mwaka

  •  Faida nyingine ya ni kuuza au kuongeza idadi.

Ukifuata utaratibu, ufugaji wa mbuzi unaweza kukuingizia kipato kizuri na kuwa biashara endelevu yenye tija.