Saturday, October 21, 2017

KILIMO CHA ZAO LA SOYA



Utangulizi:
Soya
(Glycine max) ni zao la jamii ya mikunde ambalo asili yake ni bara la Asia katika nchi ya China ambako lilianza kulimwa takribani miaka 4800 iliyopita. Zao hili liingizwa hapa nchini katika mnamo mwaka 1907 katika maeneo ya Amani wilayani Muheza katika mkoa wa Tanga. Kilimo cha zao hili kiliendelea kupanuka katika miaka ya 1930 na 1960 na kuenea katika mkoa wa Mtwara, Morogoro, na Ruvuma. Kutokana na uhamasishaji juu ya matumizi ya soya kwa lishe. Kwa sasa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji ni pamoja na Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Iringa na Morogoro. Mikoa mingine inayofaa kwa kilimo cha zao hili ni pamoja na Tanga, Lindi, Kagera, Mara, Kigoma, Kilimanjaro, Arusha na Manyara



.
Aina za soya
Zipo aina mbalimbali za soya, hapa nchini aina zinazozalishwa ni pamoja na Bossier, Uyole soya 1, Ezumu Tumu, Delma Hermon, Duiker na Kaleya. Aina hizi hutofautiana katika kustawi na kutoa mavuno hata hivyo soya aina ya Bossier huweza kustawi katika maeneo mengi zaidi hapa nchini. Mazingira yanayofaa kwa uzalishaji Soya huhitaji mvua ya kutosha ya wastani wa milimita 350 hadi 1,500 kwa mwaka inayonyesha katika mtawanyiko mzuri au umwagiliaji maji ili kuhakikisha upatikanaji wa unyevu wa kutosha kuanzia upandaji hadi inapotoa maua na matunda.
Uvunaji ni muhimu ufanyike wakati hakuna mvua ili kuruhusu soya kukauka vizuri na kutunza ubora wake.
Soya kama yalivyo mazao mengine, huhitaji udongo wenye rutuba na usiotuamisha maji. Hivyo kama shamba halina rutuba ya kutosha, ni muhimu kutumia mbolea.
Mbolea za viwandani zinazoweza kutumika ni aina ya DAP na TSP (wastani wa kilo 80 hadi 100 kwa hekta moja) kwa ajili ya kupandia na (wastani wa kilo 60 hadi 80 kwa hekta) za
mbolea ya kukuzia kama CAN. Ni muhimu kupata ushauri wa kitaalam juu ya rutuba ya udongo kabla ya kuamua kutumia mbolea.
Uzalishaji
Ni muhimu kuzingatia misimu ya mvua ya mahali husika na aina ya soya inayofaa ili kuruhusu soya kukomaa wakati hakuna mvua
na hivyo kuhifadhi ubora wake.
1. Shamba liandaliwe kwa kuondoa magugu na kutifuliwa. Soya inaweza kupandwa katika matuta au katika mistari.
2. Nafasi inayofaa katika kupanda soya ni Sm.5 hadi 10 kati ya mashina na Sm. 45 hadi 60 kati ya mstari na mstari kutegemea aina ya soya na rutuba ya udongo.
3. Kila shimo lipandwe mbegu moja katika kina cha sentimita 2 hadi tano na kufukiwa vizuri kwa udongo.
4. Palizi ifanyike kuondoa magugu, ikiwa soya itastawi na kufunika udongo vizuri inaweza kupunguza uhitaji wa kupalilia zaidi.
5. Soya huchukua wastani wa miezi mitatu hadi saba kukomaa kutegemea na aina,mahali ilikopandwa na utunzaji wa shamba.
Ni vema kuvuna soya mara inapokomaa na kuanza kukauka.
6. Soya iliyovunwa itolewe maganda na kukaushwa vizuri tayari matumizi au.kwa kuhifadhi.
7.Mavuno yanaweza kuwa kilo 1,500 hadi 2,500 kwa hekta sawa na kilo 600 hadi 1,000 kwa ekari moja kutegemea na aina na
mazingira ya uzalishaji.
Magonjwa na wadudu
Zao la soya halishambuliwi sana na magonjwa na wadudu. Inafaa kuzingatia kanuni za kilimo bora na kupata ushauri wa kitaalamu hasa inapolazimu kutumia madawa ya wadudu na magonjwa. Ni muhimu kuzingatia matumizi ya mbegu safi (zisizo na vimelea vya magonjwa) na kutumia mbinu za mzunguko wa mazao.
Maandalizi ya soya
Ni muhimu kuondoa kemikali zisizofaa kabla ya kutumia soya kwa lishe. Zingatia hatua zifuatazo:-
1. Chemsha maji
2.Tumbukiza soya kidogo kidogo ili iendeleekuchemka
3. Baada ya kuweka soya kwenye maji yanayochemka, chemsha kwa dakika 30 ili kuondoa kemikali zisizofaa.
4. Opoa, suuza na maji safi.
5. Anika hadi zikauke
6. Saga kupata unga kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Unga wa soya unaweza kutumika katika upishi wa vyakula kama vile uji, maziwa,ugali, biskuti , keki n.k
Umuhimu wa Soya
1. Soya ina viini lishe aina ya protini kwa wingi kuliko jamii zote za mikunde na hata baadhi ya protini zinazotokana na wanyama.
2. Soya ni chanzo rahisi na chenye gharama nafuu cha protini inaweza kulimwa maeneo mengi hapa nchini.
3. Kwa kuwa soya ina kiasi kikubwa cha protini kupunguza kasi ya mashambulizi ya vijidudu vya maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na magonjwa ya kansa, moyo, na kuwaongezea nguvu wagonjwa hasa wa UKIMWI;
4. Soya ni zao muhimu kwa watu wa kipato .cha chini katika kuondoa utapiamlo.
5. Kutokana na uwingi wa protini, matumizi ya soya kwa watoto
yanasaidia viungo kukua kwa haraka;
6. Soya hurutubisha udongo.
7. Soya huongeza kipato na ni zao linaloweza kuchangia katika kuondoa umaskini.
8. Utafiti unaonyesha kuwa mafuta ya soya yanaweza kutumika kwa kuendeshea mitambo yaani bio-fuel na bio-diesel

No comments:

Post a Comment