Chadema kutoa mafunzo ya M4C Kagera
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kuzindua
mafunzo ya operesheni ya vurguvugu la mabadiliko (M4C) yatakayoanza
Novemba 22 mwaka huu hadi Novemba 23 katika Wilaya ya Karagwe mkoani
Kagera.
Mafunzo hayo yatatolewa kwa wenyeviti na makatibu wa vyama hivyo ngazi
ya wilaya hadi mkoa yenye lengo la kuleta uongozi bora na kueneza sera
sahihi ya chama hicho.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
wa Mafunzo na Oganaizesheni, Benson Kigaila alisema mafunzo hayo
yamekuwa wakifanywa kwa wanachama wao ili kupata mbinu mbalimbali ya
kudai haki na uwajibikaji wa viongozi na wananchi.
“Lengo la kutoa mafunzo kwa wenyeviti na makatibu wa vyama vyetu ni
pamoja na kuwajengea uwezo wa uwajibikaji, kudai haki zao ili kuleta
hamasa kwa Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa
mabadiliko, jambo ambalo linaweza kuwapa matumaini ya maisha,”alisema
Kigaila.
Aliongeza kutokana na hali hiyo wanaamini kuwa, mabadiliko hayo yataweza
kuleta uhuru wa kweli na kubadili mfumo wa kiutawala, jambo ambalo
litaweza kuonyesha mafanikio.
Alisema kutokana na hali hiyo, jumla ya watu 64 watashiriki kwenye
mafunzo hayo yakiwamo ya darasani na vitendo ili wajumbe hao waweze
kusambaza elimu hiyo kwa wananchi katika vijiji na vitongoji,jambo
ambalo litaweza kurahisisha ufanyikaji wa mikutano ya hadhara.Alisema mbali na mafunzo hayo, kutakuwa na mikutano ya hadhara
itakayotoa mwongozo kwa viongozi hao kuonyesha uelewa wao katika mafunzo
hayo, jambo ambalo wanaamini wanaweza kufanikiwa.
Kwa mujibu wa Kigaila, Chadema inatarajia kufanya operesheni ya M4C
katika mikoa 32 na kwamba operesheni hiyo itakuwa kubwa zaidi
ikilinganishwa na zilizowahi kufanyika nchini kwa sababu tayari baadhi
ya wajumbe watakuwa na elimu ya kutosha kuhusu zoezi hilo.
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema wakati umefika kwa
sasa hapa nchini elimu ya Sekondari iwe elimu bure na kumwondolea
mwananchi wa kawaida mzigo wa kubeba gharama za elimu hiyo.
Lowassa akizungumza jana mjini Babati alisema,
mjadala kuhusu elimu kutolewa bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo
kuwataka wadau wa elimu kuanza sasa kujadili suala hilo na kwamba Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kulifanya hilo kuwa moja ya ajenda zake
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alisema elimu ya sekondari ikifanywa bure, itakuwa
ni fursa kwa kila mtoto wa Kitanzania kuipata. Hatua ambayo itaongeza
weledi na uelewa wa mambo mengi katika jamii.
“Ninasema sasa wakati umefika elimu ya sekondari
kuwa kama elimu ya msingi kwa watoto kusoma bure kuanzia kidato cha
kwanza hadi kidato cha nne,” alisisitiza Lowassa ambaye ni Mbunge wa
Monduli (CCM).
Kwa kauli hiyo, Lowassa ni kama ameunga mkono Sera
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao waliingia katika
mgogoro na CCM kuhusu elimu kutolewa bure wakati wa kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa 2010.
Chadema wamekuwa wakisisitiza kwamba elimu bure
inawezekana hadi ngazi ya sekondari, lakini wakati wote CCM wamekuwa
wakisema kuwa suala hilo haliwezekani na kwamba kauli za aina hiyo ni
kuwahadaa wananchi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, aliyekuwa mgombea wa
urais kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa alitumia sera ya elimu bure
kuanzia chekechea hadi sekondari kama kete ya kusaka ushindi, huku
akisema chama chake kingetenga asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya
kuboresha elimu na kutoa elimu bure.
Hata hivyo, aliyekuwa mgombea wa CCM na baadaye
kupata ushindi, Rais Rais Jakaya Kikwete alikuwa akiwatahadharisha
wapigakura kuwa kwamba ahadi ya Chadema ni hewa na kwamba hilo
lisingewezekana.
Mvutano huo uliwaingiza makada wengine ambao ni
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye wakati huo alikuwa Meneja
Kampeni wa CCM na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel
Sitta na kwa upande wa Chadema, Dk Kitila Mkumbo naye alijitokeza
kutetea sera ya chama chake.
Katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika
Novemba 10, 2010 katika Kata ya Mchangimbore katika Jimbo la Peramiho
mkoani Ruvuma, Rais Kikwete alisema “Serikali haiwezi kutoa huduma za
jamii bure” na kwamba lazima wananchi wachangie.
“Nimebahatika kukaa serikalini muda mrefu hiyo
sera ya bure tulijaribu na ikatushinda na wakati huo Hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Nyerere, tulikaa naye tukaona hilo haliwezekani tukaamua
tubadilishe sasa nawashangaa wenzetu wanawadanganya eti watatoa bure.”
Kwa upande wake Dk Slaa akiwa mjini Arusha katika
moja ya mikutano yake alisema kwamba CCM walikuwa wakipinga sera ya
elimu bure hadi sekondari kutokana na kulea ubadhirifu na kuthamini
anasa kuliko maendeleo kwa wananchi.
Kauli ya Lowassa
Jana
akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati,
Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo
bila ya woga.
Rais Kikwete aongoza mamia kuaga Makweta
Mbowe asema Makweta alikuwa msafi
Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda wameongoza mamia ya wakazi wa Dar es Salaam kuuaga
mwili wa mwanasiasa mkongwe, Jackson Makwetta. Mwili wa marehemu
Makwetta utasafirishwa kwa ndege leo saa 3:00 asubuhi kuelekea kijijini
kwake Njombe, baada ya kuwasili wananchi watapewa fursa ya kuuaga tena.
Wakati wa kuuaga mwili huo, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe aliitaka serikali kuchunguza miradi na mali za
viongozi kulingana na kipato walichonacho.Alisema mali alizonazo
Makwetta ni ndogo ukilinganisha na muda aliyokaa madarakani.
Mbowe
alisema baadhi ya viongozi walioko madarakani hivi sasa, wana mali
nyingi kuliko kipato chao jambo ambalo linaonyesha wazi ni mafisadi.
“Makwetta anaonyesha wazi kuwa siyo fisadi
ikilinganishwa na mali alizokuwanazo, wakati baadhi ya viongozi wa sasa
wana mali nyingi kuliko vipato vyao,” alisema Mbowe.
Alisema Makwetta amefanya kazi kwa miaka 35, lakini mali alizonazo ni ndogo, hivyo viongozi wa sasa wanapaswa kuiga mfano huo.
Naye Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema
marehemu Makweta aliwahi kuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, pia
alianzisha Mfuko wa Maendeleo Njombe ambao haujazinduliwa.
“Makwetta aliandaa mpango mkakati wa maendeleo wa Wananjombe ambao haujazinduliwa,” alisema Makinda.
Kwa upande wa Serikali mazishi hayo
yataongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Uratibu na
Sera), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Siasa), Stephen Wassira na CCM itawakilishwa na Makamu mwenyekiti wake,
Phillipo Mangula.
Marehemu Makwetta alifariki Jumamosi iliyopita
kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuhamishwa kutoka Hospitali Kuu ya
Kijeshi Lugalo. Anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwake, mkoani
Njombe.