Tuesday, November 20, 2012



 
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika 

SERIKALI ya Uswisi imeitaka Tanzania kuwasilisha kwake majina ya watu wanaotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo, kama sharti la kusaidia uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika amesema suala la kuwasilisha majina ya watuhumiwa ndilo sharti pekee ambalo Uswisi wametoa na kwamba ndiyo sababu Serikali imekuwa ikitaka wanaofahamu majina ya watuhumiwa hao wayataje.

Akizungumza jijini Mwanza jana, Mkuchika alisema ili kushughulikia suala hilo ipasavyo, Uswisi imeitaka Tanzania kuwasilisha majina ya vigogo wanaodaiwa kuficha fedha kwenye benki zake.

Alisema hayo baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Muungano wa Taasisi za Kupambana na Rushwa za Afrika Mashariki unaofanyika jijini Mwanza kwa siku mbili kuanzia jana.

Kauli hiyo ya Mkuchika imekuja siku chache baada ya kuwapo kwa taarifa zinazodai kuwa Serikali ya Uswisi imetoa masharti kwa Tanzania kuwataja wahusika walioficha fedha nje kwa majina.

Mbali na masharti hayo, Tanzania imetakiwa kuithibitishia mamlaka ya Uswisi kuwa mabilioni hayo ya fedha yametokana na rushwa na nani aliyehonga, uhamishaji wa fedha hizo, jinsi ulivyofanyika ili Serikali ya Uswisi iweze kutoa ushirikiano kusaidia kuwatia hatiani watuhumiwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuchika alisema Serikali ya Uswisi  kupitia benki zake, imetoa sharti moja tu kwa Tanzania katika kushughulikia suala hilo; kutaja majina ya watuhumiwa.

Ingawa Mkuchika hakutaja majina ya watu wanaopaswa kutaja majina ya vigogo hao, aliyewahi kujitokeza na kutoa tuhuma hizo ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Zitto alitoa kauli hizo katika Bunge la Tisa wakati akiwakilisha hoja binafsi na kulitaka Bunge kuchunguza na kuieleza Serikali ili iweze kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha nje ya nchi.

Waziri Mkuchika alisema kuwa tayari Serikali imeishatia mkono wake katika suala hilo kwa kuitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutafuta ukweli wa jambo hilo katika benki za Uswisi.

“Baada ya kumwagiza mwanasheria kufanya kazi hiyo alitekeleza na akapatiwa majibu ambayo walitoa sharti moja la kutajwa kwa majina ya vigogo hao ili waweze kuthibitisha kama watu hao walificha fedha hizo chafu katika benki zao,” alisema Mkuchika.

Alisema kuwa benki za Uswisi haziwezi kutaja  majina ya wateja wao walioweka fedha huko moja kwa moja kwa sababu ina wateja wengi raia wa Tanzania ambao wanahifadhi fedha zao huko.

Mkuchika alisema Serikali ya Tanzania imejijengea tabia ya kuwawajibisha wale wote wanaokiuka sheria za nchi na ndiyo maana katika kipindi hiki cha Awamu ya Nne sheria ya kupambana na rushwa ilijadiliwa bungeni na  baada ya kuonekana kuwa ina upungufu ikarekebishwa.

Alisema kuwa kutokana na kubadilishwa kwa sheria ya kupambana na rushwa, hivi sasa  hata mawaziri na makatibu wakuu wanawajibishwa na kuchukuliwa hatua za kisheria pindi wanapokuwa na makosa mbalimbali hivyo aliye na majina ajitokeze ili wahusika watiwe nguvuni.

Zitto anena

Hoja hiyo ya kutajwa kwa majina ya vigogo walioficha fedha Uswisi ilitokana na kauli ya Zitto hivi karibuni  bungeni  kuwalipua viongozi waandamizi wa Serikali hii wachunguzwe kutokana na makosa ya kuficha fedha nje ya nchi.

Alipotakiwa kuzungumzia kauli hiyo ya Waziri jana, Zitto alisema: “Bunge limeshaamua na kutoa maelekezo kwa Serikali kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo, waziri asibwabwaje mitaani. Anapaswa kuwa ameanza kazi. Nimeahidi ushirikiano wangu wote.”

Aliendelea: “Nina mchunguzi aliyenisaidia kufanya uchunguzi ambao nitaukabidhi kwa Serikali. Sasa hilo siyo suala la Zitto tena, kama Waziri ana maoni ayatoe bungeni, hivi sasa ni kazi na taarifa. Waziri kusemea suala hilo nje ya bunge ni contempt of Parliament,” alisema.

No comments:

Post a Comment