Tuesday, November 20, 2012



Chadema kutoa mafunzo ya M4C Kagera

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kuzindua mafunzo ya operesheni ya vurguvugu la mabadiliko (M4C) yatakayoanza Novemba 22 mwaka huu hadi Novemba 23 katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera. 

Mafunzo hayo yatatolewa kwa wenyeviti  na makatibu wa vyama hivyo ngazi ya wilaya hadi mkoa yenye lengo la kuleta uongozi bora na kueneza sera sahihi ya chama hicho.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni, Benson Kigaila alisema mafunzo hayo yamekuwa wakifanywa kwa wanachama wao ili kupata mbinu mbalimbali ya kudai haki na uwajibikaji wa viongozi na wananchi.
“Lengo la kutoa mafunzo kwa wenyeviti na makatibu wa vyama vyetu ni pamoja na kuwajengea uwezo wa uwajibikaji, kudai haki zao ili kuleta hamasa kwa Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa mabadiliko, jambo ambalo linaweza kuwapa matumaini ya maisha,”alisema Kigaila.
Aliongeza kutokana na hali hiyo wanaamini kuwa, mabadiliko hayo yataweza kuleta uhuru wa kweli na kubadili mfumo wa kiutawala, jambo ambalo litaweza kuonyesha mafanikio.

Alisema kutokana na hali hiyo, jumla ya watu 64 watashiriki kwenye mafunzo hayo yakiwamo ya darasani na vitendo ili wajumbe hao waweze kusambaza elimu hiyo kwa wananchi katika vijiji na vitongoji,jambo ambalo litaweza kurahisisha ufanyikaji wa mikutano ya hadhara.Alisema mbali na mafunzo hayo, kutakuwa na mikutano ya hadhara itakayotoa mwongozo kwa viongozi hao kuonyesha uelewa wao katika mafunzo hayo, jambo ambalo wanaamini wanaweza kufanikiwa. 
Kwa mujibu wa Kigaila, Chadema inatarajia kufanya operesheni ya M4C katika mikoa 32 na kwamba operesheni hiyo itakuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na zilizowahi kufanyika nchini kwa sababu tayari baadhi ya wajumbe watakuwa na elimu ya kutosha kuhusu zoezi hilo.

 


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema wakati umefika kwa sasa hapa nchini elimu ya Sekondari iwe elimu bure na kumwondolea mwananchi wa kawaida mzigo wa kubeba gharama za elimu hiyo.
Lowassa akizungumza jana mjini Babati alisema, mjadala kuhusu elimu kutolewa bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo kuwataka wadau wa elimu kuanza sasa kujadili suala hilo na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kulifanya hilo kuwa moja ya ajenda zake katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alisema elimu ya sekondari ikifanywa bure, itakuwa ni fursa kwa kila mtoto wa Kitanzania kuipata. Hatua ambayo itaongeza weledi na uelewa wa mambo mengi katika jamii.
“Ninasema sasa wakati umefika elimu ya sekondari kuwa kama elimu ya msingi kwa watoto kusoma bure kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne,” alisisitiza Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM).
Kwa kauli hiyo, Lowassa ni kama ameunga mkono Sera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao waliingia katika mgogoro na CCM kuhusu elimu kutolewa bure wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Chadema wamekuwa wakisisitiza kwamba elimu bure inawezekana hadi ngazi ya sekondari, lakini wakati wote CCM wamekuwa wakisema kuwa suala hilo haliwezekani na kwamba kauli za aina hiyo ni kuwahadaa wananchi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa alitumia sera ya elimu bure kuanzia chekechea hadi sekondari kama kete ya kusaka ushindi, huku akisema chama chake kingetenga asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya kuboresha elimu na kutoa elimu bure.
Hata hivyo, aliyekuwa mgombea wa CCM na baadaye kupata ushindi, Rais Rais Jakaya Kikwete alikuwa akiwatahadharisha wapigakura kuwa kwamba ahadi ya Chadema ni hewa na kwamba hilo lisingewezekana.
Mvutano huo uliwaingiza makada wengine ambao ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye wakati huo alikuwa Meneja Kampeni wa CCM na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na kwa upande wa Chadema, Dk Kitila Mkumbo naye alijitokeza kutetea sera ya chama chake.
Katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Novemba 10, 2010 katika Kata ya Mchangimbore katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, Rais Kikwete alisema “Serikali haiwezi kutoa huduma za jamii bure” na kwamba lazima wananchi wachangie.
“Nimebahatika kukaa serikalini muda mrefu hiyo sera ya bure tulijaribu na ikatushinda na wakati huo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tulikaa naye tukaona hilo haliwezekani tukaamua tubadilishe sasa nawashangaa wenzetu wanawadanganya eti watatoa bure.”
Kwa upande wake Dk Slaa akiwa mjini Arusha katika moja ya mikutano yake alisema kwamba CCM walikuwa wakipinga sera ya elimu bure hadi sekondari kutokana na kulea ubadhirifu na kuthamini anasa kuliko maendeleo kwa wananchi.
Kauli ya Lowassa
Jana akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati, Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo bila ya woga.

Rais Kikwete aongoza mamia kuaga Makweta

     Mbowe  asema Makweta alikuwa msafi


 

Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wameongoza mamia ya wakazi wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa mwanasiasa mkongwe, Jackson Makwetta.  Mwili wa marehemu Makwetta utasafirishwa kwa ndege leo saa 3:00 asubuhi kuelekea kijijini kwake Njombe, baada ya kuwasili wananchi watapewa fursa ya kuuaga tena.

Wakati wa kuuaga mwili huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliitaka serikali kuchunguza miradi na mali za viongozi kulingana na kipato walichonacho.Alisema mali alizonazo Makwetta ni ndogo ukilinganisha na muda aliyokaa madarakani.
Mbowe alisema baadhi ya viongozi walioko madarakani hivi sasa, wana mali nyingi kuliko kipato chao jambo ambalo linaonyesha wazi ni mafisadi.

“Makwetta anaonyesha wazi kuwa siyo fisadi ikilinganishwa na mali alizokuwanazo, wakati baadhi ya viongozi wa sasa wana mali nyingi kuliko vipato vyao,” alisema Mbowe.
Alisema Makwetta amefanya kazi kwa miaka 35, lakini mali alizonazo ni ndogo, hivyo viongozi wa sasa wanapaswa kuiga mfano huo.

Naye Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema marehemu Makweta aliwahi kuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, pia alianzisha Mfuko wa Maendeleo Njombe ambao haujazinduliwa.
“Makwetta aliandaa mpango mkakati wa maendeleo wa Wananjombe ambao haujazinduliwa,” alisema Makinda.

Kwa upande wa Serikali mazishi hayo yataongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Uratibu na Sera), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Siasa), Stephen Wassira na CCM itawakilishwa na Makamu mwenyekiti wake, Phillipo Mangula.

Marehemu Makwetta alifariki Jumamosi iliyopita kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuhamishwa kutoka Hospitali Kuu ya Kijeshi Lugalo. Anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwake, mkoani  Njombe.

No comments:

Post a Comment