Pwani yaelemewa na uuzaji ardhi
By Salome Kitomary ,
SOURCE:
NIPASHE
7th May 2013
Baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha KaziZumbwi,
wilayani Kisarawe mkoani Pwani. Shughuli kuu ya kiuchumi ya wakazi hao
ni kuchoma mkaa na kilimo cha mihogo.
Kasi ya uuzaji wa ardhi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, inatishia uhai wa misitu michache iliyobakia.
Unapotembelea wilaya hiyo unaona maeneo ya vichaka, misitu na mashamba
yamesafishwa kwa ajili ya kilimo. Umaskini unajidhihirisha kwa wakazi wa
eneo hilo.
Wanunuzi wa ardhi hiyo wengi wanadaiwa kutoka jijini Dar es Salaam.
Husafisha mashamba yao kwa ajili ya maandalizi ya kilimo kwa kukata
miti na kuchoma moto.
Baadhi hujipenyeza kwa mgongo wa uwekezaji na kutwaa mapande makubwa
ya ardhi na kuyaacha muda mrefu bila kuyaendeleza huku wananchi
hawaruhusiwi kuingia ndani ya eneo husika.
Kutokana na ukuaji wa miji, misitu ya mkoa wa Pwani inachukuliwa kuwa ni
mapafu ya mkoa wa Dar es Salaam , kwa ajili ya kunyoya hewa chafu
inayotokana na moshi wa magari, viwandani na shughuli za kibinadamu.
Kisayansi misitu pekee ndiyo uwezo wa kunyonya hewa chafu na kutoa hewa safi ambayo inahitajika kwa maisha ya binadamu.
Hata hivyo, wakazi wengi wa mkoa huo, shughuli kubwa za kuwaingizia
kipato vijijini ni kilimo na uchomaji mkaa, unauzwa maeneo ya miji. Jiji
la Dar es salaam linatumia
zaidi ya asilimia 90 ya mkaa unaozalishwa kwenye mistu inayokana na jiji hilo.
Hivi karibuni Waandishi wa Habari saba wa Chama cha Waandishi wa Habari
za Mazingira (Jet), walitembelea wilaya ya Kibaha na kujionea hali
halisi ya usimamizi, utunzaji wa misitu na jinsi inavyowanufasha
wanajamii.
Ziara hiyo ni sehemu ya kampeni ya Mama Misitu ambayo Jet ni
mtekelezaji ngazi ya Taifa na kubaini kasi ya uuzwaji wa ardhi
inayofanywa na wananchi kwa lengo la kujipatia kipato kwa ajili ya
maisha yao.
Uchumi wa wananchi hao ni kilimo ambacho kimeyumba kutokana na
mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira, na
kuwalazimisha wategemee uzalishaji wa mkaa na mbao na uuzaji wa ardhi
kwa wageni.
Karibu kila kijiji wilayani humo kimeuza sehemu kubwa ya ardhi, ambayo
wamiliki wapya wamesafisha kwa ajili ya kilimo kukata miti na ardhi
kubaki tupu.
Vijiji vilivyotembelewa ni Mpiji Station ambako wananchi hawana msitu wa
asili na kuibuka mgogoro baina ya mwekezaji Mohamed Enteepresies
anayemiliki eneo kubwa la ardhi, huku wananchi wakidai msitu huo ni
mali yao.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Said Mwenyedua, anasema wamesimamishwa
kufanya jambo lolote kwenye eneo hilo ambalo tangu mwaka 1974
vilivyoanzishwa vijiji walikuwa wakiulinda na kuutunza.
“Wakati tukiendelea kutunza na tukiamini ni msitu wetu, alijitokeza
mwekezaji huyo na kudai ni eneo lake, Halmashauri ilitusimamisha na
wataalamu wanafuatilia ili kujua mmiliki halisi ni nani,” alisema
Nassoro Magombe, anasema tangu alipozaliwa ameukuta msitu huo,
ameshangazwa na kauli za siku za karibuni kuwa si mali yao na
kusimamishwa wasifanye shughuli yoyote ndani yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha, Tatu Selemani, anasema
vijiji vya Kipangege, Mpiji Station na Soga, vyote vipo kwenye eneo
linalodaiwa kuwa la mwekezaji huyo.
“Tulichokifanya ni kufanya tathimini ya eneo na kumtaka Mohamed
Entepreses kuleta vithibitisho kuwa eneo ni mali yake, inaonyesha
aliuziwa chini ya sheria ya ardhi namba 5 na sasa kuna mvutano,“anasema
Anasema suala hilo limefikishwa kwa Waziri Mkuu na vijiji
hivyo vimesajiliwa vinatambulika kisheria na mvutano kuwa mkubwa kwa wananchi kuona wana haki kisheria na mwekezaji vile vile.
Anasema mwekezaji huyo kaendeleza shamba hilo kwa asilimia 15. Kati ya
ekari 20,000 ni 3,000 tu zilizopo katika kijiji cha Soga ndio
zimeendelezwa na kusababisha wananchi waamini kuwa maeneo hayo ni mali
yao.
Selemani anasema, idadi kubwa ya wanunuzi wa ardhi ni kutoka Dar es
Salaam, ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kumaliza misitu muhi mu ya
mkoa huo.
“Tunawaelimisha wananchi wasiuze ardhi ovyo, watendaji wa vijiji na kata
wamepewa barua kama kuna mtu anataka kununua ardhi watoe taarifa
wilayani, tunataka ununuzi uanzie Halmashauri ambayo ndiyo inajua
kitaalamu panapofaa kuuza kwa shughuli fulani,” anasema
Uuzaji wa ardhi kiholela anasema kuwa ni tishio kwa misitu wilayani
humo na kwa sasa utapeli wa kuuza ardhi umeingia hadi kwenye msitu wa
Serikali Kuu wa Ruvu Kusini katika eneo la Zumbamlonga ambako watu
wameuziwa ardhi.
Wauzaji hao huuza kwa bei ya kutupwa ya Sh 30,000 kwa ekari hali
inayovuta wengi na wanapouziwa hawakumbuki kwenda Halmashauri kujua
mpango wa matumizi bora ya ardhi umelelekeza nini kwenye eneo
analouziwa.
Baraza la Madiwani wameliona tatizo la uuzaji ardhi holela na kupeleka
ngazi za juu kwa ajili ya nguvu kisheria ya kuuza ardhi na si vijiji au
kata.
Wanunuzi wengi wanatoka Dar es Salaam ambako ardhi kwa ajili ya shughuli
mbalimbali hakuna. Wengine huanza kilimo na wanaokubali ushauri wa
kupanda miti hufanya
hivyo ili kulinda mazingira. Baadhi huona miti haina faida ya haraka kama mazao ya muda mfupi.
Anasema kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya
Mashariki na mashirika yasiyo ya kiserikali mojawapo likiwa mradi wa
Mama Misitu, wanaelimisha jamii kutunza mazingira kwa manufaa endelevu
na kuepukana na uuzaji ardhi kiholela ili kulinda misitu michache iliyobakia.
Kaimu Afisa Misitu wa Halmashauri ya Kibaha, Dustun Mnyenye, anasema
wanahamasisha wenye mashamba kupanda miti, lakini mwitikio ni mdogo
sana kwa
wenyeji kwa sababu wanataka faida ya haraka na baadhi ya wageni hawakubali.
Kampeni ya upandaji miti hufanyika kila mwaka kwa miti milion 1.5
hupandwa na watu binafsi ambao hupewa miti baada ya kuandaa maeneo ya
kupanda, shule za msingi na sekondari kuwa na mashamba ya miti ili
kuanzisha misitu mipya.
Kaimu Meneja Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya Mashariki, Bakari
Mohamed, anasema kasi ya uuzaji wa maeneo holela imewasukuma kuomba
kibali cha serikali kuu kuunda timu maalumu ya kufuatilia ngazi ya
vijiji na kata ili isiuzwe.
Uuzaji wa ardhi umesababisha ardhi kubaki wazi, kwani wengi husafishisha mashamba kwa madai ya kuanzisha kilimo.
Changamoto zilizopo ni mahitaji ya nishati ya mkaa kwa maeneo ya mjini
yamechangia kumaliza misitu. Kipaumbele kwenye dhana ya Kilimo Kwanza
nayo imechangia kumaliza
misitu, kwani wastaafu wengi hutumia fedha zao kununua mapande makubwa
ya ardhi na kufyeka miti na kuanzisha mashamba ya mahindi au maharagwe.
Wananchi wa maeneo hayo kwa kutojua wamejikuta wakisafisha ardhi yenye
misitu kwa ajili ya kilimo na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa
ardhi hiyo inafaa kwa kilimo.
Nyingine ni baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwa sehemu ya uharibifu wa
mazingira kwa kuingilia kati wanapokamatwa wahalifu wa uharibifu wa
misitu.
Anasema hivi karibuni walikamata kundi la ng’ombe zaidi ya 3,000 baada
ya kupigiwa simu na viongozi wa ngazi za juu serikalini na kuwataka
waachie wafugaji hiyo bila kuwatoza faini yoyote.
Nyingine ni baadhi ya wananchi kwa tama ya kipato cha haraka huingia msituni kukata miti ,kuchoma mkaa na kupasua mbao.
Anasema baadhi ya watendaji katika ngazi ya mahakama wanatumika kuharibu mazingira kwa kuwaachia wahalifu,
kutoa adhabu ndogo au kuvuruga kesi katika mazingira ya kutatanishwa na
hivyo wanaofanya vitendo hivyo kuendelea kwa kuamini wanalindwa.
Uuzwaji wa maeneo ya kando mwa bahari ya Hindi ni tatizo kubwa na
hufanywa na baadhi ya viongozi wakubwa hali inayotishia uhai wa miti
aina ya mikoko.
Anasema miti hiyo kwenye baadhi ya maeneo ya kisiwa, wananchi
wanaruhusiwa kuvuna kila baada ya muda fulani, ili kupata kipato
kutokana na hali ya maeneo yao hawana shughuli nyingine za kuingiza
kipato.
Shughuli za wakala ni ulinzi wa misitu, iliyohifadhiwa iendelee
kuhifadhiwa na kuwa na matumizi endelevu kwa ulinzi shirikishi na jamii
za maeneo husika.
Uanzishwaji wa misitu mipya kwenye maeneo mapya kama ya Rufiji, Morogoro
na Pwani, kupanda miti na kuzungusha mipaka kwenye misitu ya serikali
na kutunza miti ya mikoko.
Anasema wananchi wanashirikishwa kulinda misitu kwa kila kijiji kuwa na
kamati ya maliasili, na kuna makubalinao kwa kinachopatikana kugawanywa
kwa usawa.
Ili kuwa na uvunaji endelevu kwa kushirikiana na Mama Misitu
wameviwezesha vikundi mbalimbali vilivyopo kwenye vijiji kuwa na mizinga
ya ufugaji nyuki ili kupata kipato na kuachana na ukataji miti.
Anasema jamii inapaswa kuelewa bila misitu hakuna maisha na kutokana na
jiji la Dar es Salaam, kumaliza misitu kwa ajili ya uanzishwaji wa
makazi, tegemeo kubwa ni mkoa wa Pwani ambako misitu inakwisha.
Bila Serikali na Mamlaka zake kuingilia kati kikamilifu hali ni mbaya kwenye misitu ya jamii na ya Serikali nafanyika.
Subira Juma ni Katibu wa Kikundi cha nguvukazi Soga, ambacho
hujishughulisha na uzalishaji wa mkaa kwa kutumia nyasi, maranda na
pumba za mpunga, ambao ni mbadala wa mkaa wa miti.
Iwapo tekinolojia hiyo itawezeshwa kuwafikia wananchi wengi wataachana
na ukataji miti kwa kuwa wataweza kupata kipato kwa kuuza mkaa huo.
Wanashirikiana na jamii kulinda msitu wa Ruvu Kusini,
unaokabiliwa na wavamizi kutoka nje ya mkoa huo kwa kuvuna mbao na mkaa.