Friday, March 21, 2014

Pwani yaelemewa na uuzaji ardhi

Baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha KaziZumbwi, wilayani Kisarawe mkoani Pwani. Shughuli kuu ya kiuchumi ya wakazi hao ni kuchoma mkaa na kilimo cha mihogo.
Kasi ya uuzaji wa ardhi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, inatishia uhai wa misitu michache iliyobakia.

Unapotembelea wilaya hiyo unaona maeneo ya vichaka, misitu na mashamba yamesafishwa kwa ajili ya kilimo. Umaskini unajidhihirisha kwa wakazi wa eneo hilo.

Wanunuzi  wa ardhi hiyo wengi wanadaiwa kutoka jijini Dar es Salaam. Husafisha mashamba yao kwa ajili ya  maandalizi ya  kilimo kwa kukata miti na kuchoma moto.

Baadhi  hujipenyeza kwa mgongo wa uwekezaji na kutwaa  mapande makubwa ya ardhi na kuyaacha muda mrefu bila kuyaendeleza  huku wananchi hawaruhusiwi kuingia ndani ya eneo husika.

Kutokana na ukuaji wa miji, misitu ya mkoa wa Pwani inachukuliwa kuwa ni mapafu ya mkoa wa Dar es Salaam , kwa ajili ya kunyoya hewa chafu inayotokana na moshi wa magari, viwandani na shughuli za kibinadamu.

Kisayansi misitu pekee ndiyo uwezo wa kunyonya hewa chafu na kutoa hewa safi ambayo inahitajika kwa maisha ya binadamu.

Hata hivyo, wakazi wengi wa mkoa huo, shughuli kubwa za kuwaingizia kipato vijijini ni kilimo na uchomaji mkaa, unauzwa maeneo ya miji. Jiji la Dar es salaam linatumia
zaidi ya asilimia 90 ya mkaa unaozalishwa kwenye mistu inayokana na jiji hilo.

Hivi karibuni Waandishi wa Habari saba wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (Jet), walitembelea wilaya ya Kibaha na kujionea hali halisi ya usimamizi, utunzaji wa misitu na jinsi inavyowanufasha wanajamii.

Ziara hiyo ni sehemu ya  kampeni ya Mama Misitu ambayo Jet ni mtekelezaji ngazi ya Taifa na kubaini  kasi ya uuzwaji wa ardhi inayofanywa na wananchi kwa lengo la kujipatia kipato kwa ajili ya maisha yao.

Uchumi wa wananchi hao ni kilimo ambacho kimeyumba kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira, na kuwalazimisha wategemee uzalishaji wa mkaa na mbao na uuzaji wa ardhi kwa wageni.

Karibu kila kijiji wilayani humo kimeuza sehemu kubwa ya ardhi, ambayo wamiliki wapya wamesafisha kwa ajili ya kilimo  kukata miti na ardhi kubaki tupu.

Vijiji vilivyotembelewa ni Mpiji Station ambako wananchi hawana msitu wa asili na kuibuka mgogoro baina ya mwekezaji Mohamed Enteepresies anayemiliki  eneo kubwa la ardhi, huku wananchi wakidai msitu huo ni mali yao.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Said Mwenyedua, anasema wamesimamishwa kufanya jambo lolote kwenye eneo hilo ambalo tangu mwaka 1974 vilivyoanzishwa vijiji walikuwa wakiulinda na kuutunza.

“Wakati tukiendelea kutunza na tukiamini ni msitu wetu, alijitokeza mwekezaji huyo na kudai ni eneo lake, Halmashauri ilitusimamisha na wataalamu wanafuatilia ili kujua mmiliki halisi ni nani,” alisema

Nassoro Magombe, anasema tangu alipozaliwa  ameukuta msitu huo, ameshangazwa na kauli za siku za karibuni kuwa si mali yao na kusimamishwa wasifanye shughuli yoyote ndani yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha, Tatu Selemani, anasema vijiji vya Kipangege, Mpiji Station na Soga, vyote vipo kwenye eneo linalodaiwa kuwa la mwekezaji huyo.

“Tulichokifanya ni kufanya tathimini ya eneo na kumtaka Mohamed Entepreses kuleta vithibitisho kuwa eneo ni mali yake, inaonyesha aliuziwa chini ya sheria ya ardhi namba 5 na sasa kuna mvutano,“anasema

Anasema suala hilo limefikishwa  kwa Waziri Mkuu na vijiji
hivyo vimesajiliwa vinatambulika kisheria na mvutano kuwa mkubwa kwa wananchi kuona wana haki kisheria na mwekezaji vile vile.

Anasema mwekezaji huyo kaendeleza shamba hilo kwa asilimia 15. Kati ya ekari 20,000 ni  3,000 tu zilizopo katika  kijiji cha Soga ndio zimeendelezwa  na kusababisha wananchi waamini kuwa maeneo hayo ni mali yao.

Selemani anasema, idadi kubwa ya wanunuzi wa ardhi ni kutoka Dar es Salaam, ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kumaliza misitu muhi mu ya mkoa huo.

“Tunawaelimisha wananchi wasiuze ardhi ovyo, watendaji wa vijiji na kata wamepewa barua kama kuna mtu anataka kununua ardhi watoe taarifa wilayani, tunataka ununuzi uanzie Halmashauri ambayo ndiyo inajua kitaalamu panapofaa kuuza kwa shughuli fulani,” anasema

Uuzaji wa ardhi kiholela  anasema kuwa ni tishio kwa misitu wilayani humo na kwa sasa utapeli wa kuuza ardhi umeingia hadi kwenye msitu wa Serikali Kuu wa Ruvu Kusini katika eneo la Zumbamlonga ambako watu wameuziwa ardhi.

Wauzaji hao huuza kwa bei ya kutupwa ya Sh 30,000 kwa ekari hali  inayovuta wengi na wanapouziwa hawakumbuki kwenda Halmashauri kujua mpango wa matumizi bora ya ardhi umelelekeza nini kwenye eneo analouziwa.

Baraza la Madiwani wameliona tatizo la uuzaji ardhi holela na kupeleka ngazi za juu kwa ajili ya  nguvu kisheria ya kuuza ardhi na si vijiji au kata.

Wanunuzi wengi wanatoka Dar es Salaam ambako ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali hakuna. Wengine huanza kilimo na wanaokubali ushauri wa kupanda miti hufanya
hivyo ili kulinda mazingira. Baadhi huona miti haina faida ya haraka kama mazao ya muda mfupi.

Anasema kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya Mashariki na mashirika yasiyo ya kiserikali mojawapo likiwa mradi wa Mama Misitu, wanaelimisha jamii kutunza mazingira kwa manufaa endelevu
na kuepukana na uuzaji ardhi kiholela ili kulinda misitu michache iliyobakia.

Kaimu Afisa Misitu wa Halmashauri ya Kibaha, Dustun Mnyenye, anasema wanahamasisha wenye mashamba kupanda miti, lakini  mwitikio ni mdogo sana kwa
wenyeji kwa sababu wanataka faida ya haraka na baadhi ya wageni hawakubali.

Kampeni ya upandaji miti hufanyika kila mwaka kwa miti milion 1.5 hupandwa na  watu binafsi ambao hupewa miti baada ya kuandaa maeneo ya kupanda, shule za msingi na sekondari kuwa na mashamba ya miti ili kuanzisha misitu mipya.

Kaimu Meneja Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya Mashariki, Bakari Mohamed, anasema kasi ya uuzaji wa maeneo holela imewasukuma kuomba kibali cha serikali kuu kuunda timu maalumu ya kufuatilia ngazi ya vijiji na kata ili isiuzwe.

Uuzaji wa ardhi umesababisha ardhi kubaki wazi, kwani wengi husafishisha mashamba kwa madai ya kuanzisha kilimo.

Changamoto zilizopo ni mahitaji ya nishati ya mkaa kwa maeneo ya mjini yamechangia kumaliza misitu. Kipaumbele kwenye dhana ya Kilimo Kwanza nayo imechangia kumaliza
misitu, kwani wastaafu wengi hutumia fedha zao kununua mapande makubwa ya ardhi na kufyeka miti na kuanzisha mashamba ya mahindi au maharagwe.

Wananchi wa maeneo hayo kwa kutojua wamejikuta wakisafisha ardhi yenye misitu kwa ajili ya kilimo na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa ardhi hiyo  inafaa kwa kilimo.

Nyingine ni baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwa sehemu ya uharibifu wa mazingira kwa kuingilia kati  wanapokamatwa wahalifu wa uharibifu wa misitu.

Anasema hivi karibuni walikamata kundi la ng’ombe zaidi ya 3,000 baada ya  kupigiwa simu na viongozi wa ngazi za juu serikalini na kuwataka waachie wafugaji hiyo bila kuwatoza faini yoyote.

Nyingine ni baadhi ya  wananchi  kwa tama ya kipato cha haraka huingia msituni  kukata miti ,kuchoma mkaa na kupasua mbao.

Anasema  baadhi ya watendaji katika ngazi ya mahakama wanatumika kuharibu mazingira kwa kuwaachia wahalifu,

kutoa adhabu ndogo au kuvuruga kesi katika mazingira ya kutatanishwa na hivyo wanaofanya vitendo hivyo kuendelea kwa kuamini wanalindwa.

Uuzwaji wa maeneo ya kando mwa bahari ya Hindi ni tatizo kubwa na hufanywa na  baadhi ya viongozi wakubwa hali inayotishia uhai wa miti aina ya mikoko.

Anasema miti hiyo kwenye baadhi ya maeneo ya kisiwa, wananchi wanaruhusiwa kuvuna kila baada ya muda fulani, ili kupata kipato kutokana na hali ya maeneo yao hawana shughuli nyingine za kuingiza kipato.

Shughuli za wakala ni ulinzi wa misitu, iliyohifadhiwa iendelee kuhifadhiwa na kuwa na matumizi endelevu kwa ulinzi shirikishi na jamii za maeneo husika.

Uanzishwaji wa misitu mipya kwenye maeneo mapya kama ya Rufiji, Morogoro na Pwani, kupanda miti na kuzungusha mipaka kwenye misitu ya serikali na kutunza miti ya mikoko.

Anasema wananchi wanashirikishwa kulinda misitu kwa kila kijiji kuwa na kamati ya maliasili, na kuna makubalinao kwa kinachopatikana kugawanywa kwa usawa.

Ili kuwa na uvunaji endelevu kwa kushirikiana na Mama Misitu
wameviwezesha vikundi mbalimbali vilivyopo kwenye vijiji kuwa na mizinga ya ufugaji nyuki ili kupata kipato na kuachana na ukataji miti.

Anasema jamii inapaswa kuelewa bila misitu hakuna maisha na kutokana na jiji la Dar es Salaam, kumaliza misitu kwa ajili ya uanzishwaji wa makazi, tegemeo kubwa ni mkoa wa Pwani ambako misitu inakwisha.

Bila Serikali na Mamlaka zake kuingilia kati kikamilifu hali ni mbaya kwenye misitu ya jamii na  ya Serikali nafanyika.

Subira Juma ni Katibu wa Kikundi cha nguvukazi Soga, ambacho hujishughulisha na uzalishaji wa mkaa kwa kutumia nyasi, maranda na pumba za mpunga, ambao ni mbadala wa mkaa wa miti.

Iwapo tekinolojia hiyo itawezeshwa kuwafikia wananchi wengi wataachana na ukataji miti kwa kuwa wataweza kupata kipato kwa kuuza mkaa huo.

Wanashirikiana na jamii kulinda msitu wa Ruvu Kusini,
unaokabiliwa na wavamizi kutoka nje ya mkoa huo kwa kuvuna mbao na mkaa.

No comments:

Post a Comment