Thursday, January 1, 2015


Mwaka mpya wa 2015 ulioingia saa 6:00 usiku wa kuamkia leo January 01, unatarajiwa kuwa na matukio muhimu na yenye mvuto mkubwa kisiasa, mojawapoa likiwa ni uchaguzi mkuu.
Uchaguzi huo utahusisha nafasi za Udiwani, Ubunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu 2015.

Uchaguzi huo, ambao utahitimisha miaka 10 ya vipindi viwili vya uongozi wa Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ulioanzia mwaka 2005.

Pia unahitimisha miaka mitano ya uongozi wa Rais wa sasa wa SMZ, Dk. Ali Mohammed Shein, ulioanzia mwaka 2010.

Vilevile, unahitimisha kipindi cha wabunge na madiwani cha miaka mitano ya kuwawakilisha wananchi bungeni.

Unafuatia uchaguzi wa mwisho chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini, uliofanyika mwaka 2010.

KATIKA SALAMA ZAKE ZA KUMALIZA MWAKA 2014 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2015, Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete amelihutubia Taifa, Tarehe 31 Desemba, 2014 na kuzichambua sekta mbalimbali kama vile za Elimu, Ujenzi wa maabara, Umeme, Chakula, mfumuko wa Bei, Ujangili, Dawa za kulevya, mapato ya Serikali, Dawa za kulevya na mapato ya Serikali. 
Rais akihitimisha salama zake akisema,’’-

Ndugu Wananchi;

Namaliza hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa kuiunga mkono Serikali yetu na kwa mchango wenu uliowezesha nchi yetu kupata mafanikio haya makubwa tunayojivunia katika mwaka 2014. Tumeweza kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu mengi. 

Umoja wetu na mshikamano wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza mwaka 2015 kwa matumaini makubwa. 

Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya kuendelea kuliimarisha zaidi taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo huenda ukawa na changamoto na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka huu. 

Uelewa wetu, umoja wetu, mshikamano wetu na moyo wetu wa uzalendo ndivyo vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. Mimi nina imani kubwa kwa uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa nzuri ya nchi yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na utulivu. 

Tumeweza mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na miaka ijayo. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka mpya.

Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania!

Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment