Thursday, January 1, 2015

Rais Xi Jinping wa China atoa salamu za mwaka mpya 2015

(GMT+08:00) 2014-12-31 19:42:15



Rais Xi Jinping wa China Desemba 31 2014 ametoa salamu za mwaka mpya na kuwatakia marafiki waliopo katika sehemu mbalimbali duniani heri ya mwaka mpya wa 2015. Salamu hizo zimerushwa hewani kupitia Radio China Kimataifa CRI, Radio ya taifa ya China CNR na Televisheni ya taifa ya China CCTV. Zifuatazo ni salamu za rais Xi Jinping.
Muda unapita haraka, umebaki muda mfupi kabla ya kuuaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015. Kwa dhati ya moyo, nawatakia kila la heri wananchi wenzangu, ndugu wa mikoa ya utawala maalumu ya Hong Kong na Macao, ndugu wa Taiwan na wachina walioko ng'ambo, pamoja na marafiki wa nchi na sehemu mbalimbali duniani.
Mwaka 2014 ni mwaka usiosahaulika. Mwaka huu, China ilidhamiria kusukuma mbele mageuzi, na kufanikiwa kutatua baadhi ya matatizo magumu, ambapo tuliweka hatua mbalimbali muhimu za mageuzi, ambazo nyingi zinahusiana kwa karibu na maslahi ya wananchi. Tumejitahidi kuhimiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na juhudi hizo zimeleta mabadiliko mapya kwa maisha ya wananchi. Tarehe 12 Desemba, mradi mkubwa wa kujenga mifereji ya kusafirisha maji kutoka kusini hadi kaskazini mwa China ulikamilika kwa kipindi cha kwanza, wachina zaidi ya laki 4 waliokuwa wanaishi kwenye sehemu mifereji hiyo inazopita wamehamishwa. Tunapaswa kuwashukuru kutokana na mchango wa mkubwa waliotoa kwa ajili ya mradi huo. Nawatakia maisha ya furaha na neema katika makazi mpya. Mwaka 2014, tumeweka mkazo katika kulinda nidhamu na maadili serikalini, haswa kupambana na vitendo vya kulipua kazi na uzembe kazini, pamoja na hali ya kuendekeza raha na maisha ya anasa. Hivi sasa hali imeboreshwa kidhahiri.Tumeongeza nguvu katika kupambana na ufisadi, na kuwaadhibu vikali maofisa waliohusika na ufisadi, hali ambayo imeonesha nia yetu thabiti ya kuondoa tatizo hilo. Mwaka 2014, tuliimarisha mawasiliano na ushirikiano na nchi mbalimbali duniani, tuliandaa mkutano usio rasmi wa viongozi wa Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya Asia na Pasifiki APEC. Viongozi wa China na nchi za nje walitembeleana mara kwa mara. Shughuli hizo zimetangaza China vizuri zaidi duniani.
Ili kufanikisha kazi hizo, maofisa wa China katika ngazi mbalimbali walichapa kazi kwelikweli. Ni hakika kuwa kazi hizo hazikuweza kufanikiwa bila uungaji mkono wa umma, kwa hiyo napenda kuwapongeza na kuwashukuru wananchi wenzangu.
Mwaka 2014, tuliweka kisheria Siku ya ushindi wa vita dhidi ya uvamizi wa Japan, Siku ya mashujaa na Siku ya taifa ya kuwaomboleza waliouawa na kuathiriwa katika mauaji ya halaiki ya Nanjing. Tulifanya maadhimisho katika siku hizo. Ni lazima tuwakumbuke daima watu walijitoa muhanga kwa ajili ya taifa na amani.
Mwaka 2014, pia tulikumbwa na matukio ya kuhuzunisha. Ndege ya abiria ya Shirika la ndege la Malaysia MH370 ilipotea na ndugu zetu zaidi ya 150 hawajulikani walipo, hatuwezi kuwasahau, tunapaswa kuendelea na juhudi za kuwatafuta. Mwaka 2014, China ilikumbwa na maafa na ajali mbalimbali, ambazo ndugu wengi walipoteza maisha. Tetemeko la ardhi lililotokea mjini Ludian mkoani Yunnan lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 600, tunawakumbuka na kuwatakia heri ndugu na jamaa zao.
Kengele ya mwaka mpya inakaribia kugonga. Tunapaswa kuendelea kufanya juhudi, ili kutekeleza kivitendo matarajio na matumaini ya wananchi. Tutaendelea kuimarisha mageuzi bila kusita na kuyafanikisha kwa ushupavu. Tutahimiza kwa pande zote utawala kwa mujibu wa sheria, ili kulinda maslahi ya wananchi, kutetea haki na usawa katika jamii na kuhimiza maendeleo ya taifa. Mageuzi na utawala kwa mujibu wa sheria ni mambo yasiyotengana kama mabawa mawili ya ndege na magurudumu mawili ya gari, ambayo yanatusaidia katika kutimiza lengo la kujenga jamii yenye maisha bora.
Kwa jumla, maisha ya watu wa China yanaboreshwa siku hadi siku, lakini siku zote tunapaswa kuwafuatilia watu wenye matatizo ya kimaisha. Tunatakiwa kuwa na shauku katika kazi za kuboresha maisha ya umma, haswa kazi ya kuondoa umaskini pamoja na kuweka uhakikisho wa maisha ya kimsingi, ili watu wote wanaohitaji misaada waweze kujikimu kimaisha na kuwa na upendo mioyoni.
Tunapaswa kuendelea na kazi ya kuimarisha nidhamu ya chama chetu, kuendelea kuweka mkazo kwenye mapambano dhidi ya ufisadi na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya madaraka. Katika nchi yetu ya kisoshalisti inayoongozwa na chama cha kikomunisti cha China, mtu yeyote anayethibitishwa kujihusisha na ufisadi, ni lazima aadhibiwe.
Kazi tunayoendelea nayo ni kubwa, ushindi utapatikana tu kutokana na juhudi thabiti zenye uvumilivu, kama tukisitasita njiani hakika tutarudi nyuma. Mpango wetu ni mkubwa, hivyo juhudi zinazotakiwa kuufanikisha zitakuwa kubwa na ngumu. Wanachama na wananchi wa makabila yote wanatakiwa kushikamana kwa moyo mmoja, kutumia vizuri fursa zinazoibuka kwa kukusanya busara za umma, kukabiliana na changamoto zinazotokea kwa nia ya pamoja, kutatua masuala magumu kwa hatua madhubuti na zaharaka, na kufanya uvumbuzi kwa bidii, ili kuhimiza maendeleo ya nchi na maisha ya wananchi yapige hatua mwaka hadi mwaka.
Watu wa China wanafuatilia mustakbali wa nchi yetu, na pia wanafuatilia mustakbali wa dunia nzima. Mlipuko wa Ebola ulipotokea Afrika, tulitoa misaada. Huduma ya maji ya kunywa ilipokatika nchini Maldives, tulipeleka maji. Shughuli mbalimbali kama hizo zimeonesha urafiki mkubwa kati ya watu wa China na watu wa nchi mbalimbali duniani. Dunia ya hivi leo bado inakabiliwa na machafuko mbalimbali. Tunatoa wito wa amani na kutumai kwa dhati kuwa watu wa nchi zote duniani watafanya juhudi za pamoja ili watu wote wasisumbuliwe na baridi na njaa, familia zote zisitishiwe na vita, na watoto wote waweze kukua katika mazingira ya amani.
Asanteni sana.

No comments:

Post a Comment