Sunday, March 16, 2014



Jana March 13 kupitia vyombo mbalimbali vya habari ilitoka stori iliyowahusisha Wagombea Ubunge jimbo la Chalinze ambao ni Fabian Leonard Skauki wa CUF na Matheo wa  Chadema juu ya kusemekana kuwa Mathayo Mang’unda Torongey aliongopa kwenye ujazaji wa fomu zake za kugombea Ubunge jimbo hilo.

Leo millardayo.com imefika tena hadi Bagamoyo makao makuu ya wilaya Chadema kwa ajili ya kufahamu undani wa madai hayo ya Mgombea wa Cuf ambapo Matheo ameanza kwa kusema>>’kwanza labda niweke sawa zile fomu hakuna sehemu ambayo inasema uambatanishe na vielelezo vya shughuli unayofanya’
MATHEO
‘Kiuhalisia mimi ni mfanyabiashara wa siku nyingi nafanya biashara na maduka ya nyama kuhusu kughushi sahihi ya wadhamini hili ni suala ambalo sio la ukweli kwa sababu wakati  tunarudisha fomu ilihakikiwa na mkurugenzi ambae ndiye msimamizi wa uchaguzi’
‘Na sio saini za mkono peke yake zipo za dole gumba na zipo mchanganyiko na tunazo pia zile shahada za wapiga kura,tulifanya uhakiki na shahada zenyewe hivyo mkurugenzi alihakiki na kusema zipo sawa sawa’

‘Kuhusu kusema kuwa mimi sio Mtanzania hilo suala sio la kwangu nafikiri la uhamiaji au wanalo wenyewe lakini mimi ni Mtanzania halalai na ninacho kitambulisho cha kupigia kura ambacho nafikiri watanzania wengi wanakitumia’
CHANZO:MILLARDAYO.COM


Mgombea Chadema Chalinze apingwa

By Waandishi wetu;   14th March 2014

Mgombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze, Pwani kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Fabian Skauki, amemwekea pingamizi mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mathayo Torongey kwa msimamizi wa uchaguzi, akisema hana sifa za kugombea.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo zililifikia NIPASHE jana, mgombea wa CUF ametaja sababu kadhaa zilizomfanya amwekee pingamizi mgombea wa Chadema kuwa ni pamoja na kutojua kusoma na kuandika lugha za Kiswahili na Kiingereza.

Katika pingamizi hilo ambalo liliwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Chalinze, Skauki alidai kuwa mgombea huyo wa Chadema amejaza katika fomu kwamba anajua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza wakati ni uongo.

“Mgombea wa Chadema amejaza katika fomu kwamba anajua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza wakati ni uongo, hajui kusoma wala kuandika Kiswahili wala Kiingereza, amedanganya na amepoteza sifa za kuwa mgombea,” alisema Skauki katika pingamizi hilo.

Sababu nyingine iliyoelezwa ni kwamba mgombe wa Chadema amedanganya kwa kughushi sahihi za wadhamini, ambao amewaorodhesha kwenye fomu ya kuomba kuthibitishwa kuwa mgombea.

Alidai kuwa katika fomu hizo wadhamini wote na sahihi zao zimeghushiwa na hazifanani na kwamba zile zilizokuwapo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura sahihi zote zimesainiwa na mtu mmoja ambaye siyo mhusika.

Sababu ya nne ni kwamba mgombea wa Chadema ameshindwa kutimiza mahitaji ya kisheria ya kuwa na wadhamini wasiopungua 25, badala yake amedhaminiwa na wadhamini 28 ambao kati yao wadhamini saba siyo wapiga kura halali wa jimbo la Chalinze, hivyo wadhamini halali ni 21 ambao hawafikii idadi  inayotakiwa.

Kadhalika, Skauki anadai katika pingamizi lake dhidi ya mgombea wa Chadema kwamba katika fomu zake alisema kuwa shughuli anazojihusisha nazo ni biashara, lakini hakuonyesha vielelezo kuthibitisha.

Vile vile, Skauki anadai kwamba Torongey siyo raia wa kuzaliwa Tanzania kwa kuwa hakuna vielelezo alivyowasilisha kuthibitisha kama ni raia wa kuzaliwa.

Baada ya kutoa tuhuma hizo, aliiomba Tume ya Uchaguzi (NEC) kutengua uteuzi wa Torongey kwa kuwa anakosa sifa za kuendelea kuwa mgombea.

Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi jimbo la Chalinze, Hoza Mohamed, alithibitisha kupokea pingamizi la mgombea wa CUF na kusema kwamba ofisi ya msimamizi inashughulikia suala hilo kwa ajili ya kutoa maamuzi.

“Ni kweli nimepokea pingamizi kwa niaba ya msimamizi wa uchaguzi na hivi sasa tunalifanyia kazi,” alisema Mohamed.

Hata hivyo, Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Nickson Tugara, alikanusha tuhuma hizo na kusema kuwa mgombea wa CUF anatapatapa kwa vile anajua nafasi hiyo itachukuliwa na Chadema.

“Sisi hatujaweka wadhamini mamluki, bali ni watu wenye sifa ambao wako kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na pia Chadema imefuata taratibu zote kwa kwenda mahakamaani na Halmashauri ya Bagamoyo kuwalipia gharama za fomu,” alisema Tugara.

Alisema kuwa majina ya wadhamini na sura zao zipo kwenye kompyuta za halmashauri, hivyo anachofanya mgombea kupitia CUF ni kutapatapa na hajui taratibu za kisheria zinavyokwenda.

“Mgombea wetu anajua kusoma na kuandika na ana sifa zote za kuwania nafasi hiyo, ila CUF wamepanga kumchafua na hawataweza kwani Chadema tuko makini tunaposimamia mambo yetu na tutazindua kampeni zetu Machi 16,” alisema.

Meneja kampeni wa mgombea wa Chadema, John Mrema, alisema wamepata taarifa za kuwekewa pingamizi mgombea wao, lakini alisema ofisi ya msimamizi wa uchaguzi bado haijatoa taarifa rasmi kwa Chadema.

Mgombea mwingine katika uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika Aprili 6, mwaka huu ni Ridhiwani Kikwete kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo Januari 22, mwaka huu.
SOURCE: NIPASHE




No comments:

Post a Comment