Uamuzi wa kuambatana na viongozi wastaafu wa
kitaifa unatafsiriwa na wengi kama ishara ya kuupa uzito mchakato wa
Katiba Mpya na uhalali wa kisiasa na kuleta umoja na utengamano miongoni
mwa makundi ya wajumbe wanaounda Bunge hilo la kihistoria.
Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa mjadala
katika Bunge hilo, kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji sababu za Jaji
Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni juzi kabla ya Rais kuzindua
Bunge kama Kanuni zinavyoelekeza.
Itakumbukwa kwamba mjadala huo ulizua mtafaruku
baada ya baadhi ya wajumbe kumzuia Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo
Jumatatu iliyopita hadi kilipofanyika kikao cha maridhiano usiku wa siku
hiyo na kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba awasilishe Rasimu hiyo juzi na Rais ahutubie Bunge leo.
Mabishano hayo yalitokana na baadhi ya wajumbe
kujenga dhana kwamba ukiukwaji huo wa Kanuni ulilenga kumpa Rais fursa
ya kujibu mapigo na kupangua hoja za Jaji Warioba kutokana na wajumbe
wengi wa chama chake cha CCM kuonyesha wazi kupinga na kubeza
mapendekezo nyeti yaliyomo kwenye Rasimu hiyo, ambayo Jaji Warioba
aliiwasilisha bungeni kwa ufasaha, umakini na ustadi mkubwa kiasi cha
kuwafungua macho wengi, hasa pale alipowafafanulia mambo mengi ambayo
wamekiri walikuwa hawayafahamu wala kuyaelewa.
Tunaupongeza uongozi wa Bunge na wajumbe wote kwa
jumla kwa kutumia busara na kuendelea na shughuli za Bunge ambazo
zilikuwa zimesimama. Vinginevyo, Bunge lingesambaratika na kufuta ndoto
za wananchi za kupata Katiba Mpya inayokubalika kwa wengi. Hata hivyo,
mtafaruku huo ulitoa somo kwa uongozi wa Bunge kwamba Bunge hilo
lisipoendeshwa kwa kufuata na kuheshimu Kanuni zilizowekwa,
litasambaratika.
- Mheshimiwa Rais anatarajiwa kuambatana na viongozi wastaafu wa kitaifa kama ishara ya kuupa uzito mchakato wa Katiba Mpya na uhalali wa kisiasa na kuleta umoja na utengamano miongoni mwa makundi ya wajumbe wanaounda Bunge hilo la kihistoria
Pamoja na kutoa pongezi hizo, tungependa kumshauri
Rais Kikwete atambue kwamba leo atakuwa akilihutubia Bunge ambalo
wajumbe wake wamegawanyika, hasa kutokana na msimamo wa CCM wa kuvikataa
vifungu muhimu vya Rasimu ya Katiba. Tunasema hivyo baada ya viongozi
na wajumbe wengi wa CCM kutoa kauli za kuendeleza misimamo mikali
inayokinzana na maoni yaliyotolewa na wananchi na kuingizwa kwenye
Rasimu hii ya Katiba.
Hotuba ya Rais inaweza kugusia maudhui yaliyomo
katika Rasimu ya Katiba, lakini tunadhani kufanya hivyo itakuwa kosa
kubwa kwa kua atakuwa ameingia katika mtego wa kujibu hoja zilizomo
katika hotuba ya Jaji Warioba aliyoitoa juzi bungeni. Akifanya hivyo
atakuwa analiingiza Bunge katika sintofahamu itakayolisambaratisha,
kwani yeye si sehemu ya Bunge, bali atakwenda pale kama mkuu wa nchi.
Kwa maana hiyo, hatutarajii alihutubie Bunge
kuelezea misimamo yake binafsi au misimamo ya chama chake cha CCM au
kundi jingine lolote lile.
Hivyo, atafanya vyema iwapo atakwenda pale kama
kiunganishi muhimu cha makundi yote yaliyo bungeni. Tunadhani umoja,
utengamano na nia ya serikali yake kuhakikisha Katiba Mpya inayokubalika
kwa wengi inapatikana katika muda uliopangwa ndio mambo muhimu na ambao
utalinusuru Bunge la Katiba.
No comments:
Post a Comment