Chadema yaahidi amani, maendeleo Chalinze Ijumaa, Marchi21
2014
saa
11:40 AM
- Waeleza mikakati yao na kuwaomba wafuasi wao kuepuka vurugu.
Bagamoyo. Mwenyekiti wa Baraza
la Vijana (Chadema) Mkoa wa Pwani, Elison Kinyaha amesema ili kudumisha
maendeleo, upendo na amani ndani ya Jimbo la Chalinze, upo ulazima wa
wakazi wa jimbo hilo kumchagua Mathayo Torongey katika uchaguzi mdogo
unaotarajia kufanyika mapema Aprili 6, mwaka huu.
Kinyaha alisema kutokana na uelewa mpana wa wakazi
wa jimbo hilo ni wazi kuwa chama hicho ndicho kinachoweza kuibuka na
ushindi kwani mtu anayegombea nafasi hiyo ni mpigania haki za wanyonge
na anayetambua shida zinazowakabili kwa kipindi kirefu.
Alisema kumpitisha mgombea huyo hawakukurupuka
bali walitumia utashi na heshima kubwa iliyomo ndani ya uongozi wa
Chadema, hivyo mpaka sasa wanatambua kuwa, kazi wanayoifanya sasa ya
kampeni si ya kubahatisha bali ni kushika uongozi wa ubunge ndani ya
Jimbo la Chalinze.
“Sisi leo tuko Kata ya Pera na Kijiji cha
Chamakweza, tukiendelea na kampeni ambayo tuliizindua tangu Jumapili.
Kikubwa ni kuzungumza na wananchi kwa ustaarabu na kuwajulisha chama
wanachopaswa kukichagua ambacho ni Chadema pekee kinachojali shida za
wanyonge,”
Alisema kuwa katika kipindi kifupi tangu chama hicho kilipozindua kampeni, hali ya mwitikio imekuwa ya kutia matumaini hususan katika mahudhurio ya kampeni kwenye maeneo mbalimbali na kudai hilo linaonyesha ni kukubaliwa kwa sera za chama hicho ambazo zaidi zinajikita kwenye kutetea wanyonge na usawa.
Alisema katika zoezi zima la kampeni, chama chao
kitafanya kazi hiyo kwa ustaarabu na kuepusha vurugu na ni imani yake
wana Chadema wote watajiepusha na hali yoyote inayoweza kutokea kwa
upande wa vyama vingine.
Wakati huohuo juzi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Mwantumu Mahiza alisema katika kuhakikisha Uchaguzi wa Jimbo la Chalinze
unafanyika kwa amani na utulivu ni vyema viongozi wa dini zote
wakafanya maombi kwa Mungu.
Alisema viongozi hao wanayo nafasi kubwa kutokana
na imani tangu enzi na kuwataka kuhubiri mema kwa waumini wao ambao
wengi ni wafuasi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo mdogo.
“Ndugu zangu viongozi wa dini, msijisahau katika
maombi yenu ombeeni na huu uchaguzi mdogo utakaofanyika mapema mwezi
ujao ili haki, amani na hekima itawale kwenye zoezi zima la kazi hiyo
muhimu,” alisema.
No comments:
Post a Comment