Friday, March 14, 2014




MATREKTA KWA AJILI YA KUFANIKISHA SHUGHULI ZA KILIMO

Wabunge 42 Chadema kufunika kalenga

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo vimeendelea kuchuana katika wiki ya lala salama ya kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga, Iringa kwa kumwaga makada wa kitaifa na vijana wa kulinda kura.

 Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema,Freeman Mbowe na wabunge 42 wa chama hicho wameitwa na Katibu Mkuu wake,  Dk. Willibrad Slaa, kuongeza nguvu kwenye kata 13 za jimbo hilo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge Jumapili ijayo.

Meneja kampeni wa chama hicho na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, akizungumza jana wakati akimnadi mgombea wa chama chake, Grace Tendega, katika Kijiji cha Magulilwa alisema uamuzi huo unalenga kupambana na hujuma za wizi wa kura unaoweza kufanywa na mahasimu wao kisiasa.

“Mwenyekiti na wabunge wengine 42 kesho (leo) watakuwa  wameshasambazwa kila kata ya jimbo hili kwa ajili ya kuongeza nguvu. Hawa CCM bila kuwadhibiti kwa staili hiyo watatuumiza. Kwa hiyo tayari Dk. Slaa ameshawaita na mtakutana nao huko kwenye maeneo yenu wakiwaomba mumchague Tendega (Grace) kuwawakilisha bungeni,” alisema Lema.

Alisisitiza kwamba ili kuhakikisha Tendega anatwaa kiti hicho, wabunge wenzake wamechangishana kila mmoja Sh. milioni mbili kwa ajili ya kumwongezea nguvu ya kupambana na mahasimu wake kisiasa.

MANGULA KUONGOZA CCM

Wakati Chadema ikiongeza nguvu, wapinzani wao CCM, wamesema hawana mpango wa kuongeza wapiganaji kutoka nje ya mkoa wa Iringa kwa kuwa makada pamoja na vikosi vyake ambavyo kwa sasa vinaongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula, vina uwezo mkubwa wa kukabiliana na wabunge, makada na wafuasi wa Chadema.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye, aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu jana kwamba hawana mpango wa kuongeza nguvu wala kukodi watu kutoka mikoa mingine ili kukabiliana na wapinzani wao katika wiki ya lala salama kuelekea uchaguzi huo.

“Mzee Mangula anatosha kuwaumbua Chadema katika uchaguzi wa Kalenga kwa sababu anayo timu iliyokamilika huko Kalenga na hatuna sababu ya kuongeza nguvu kama Chadema wanavyofanya hivi sasa. Nawahakikishia Watanzania kwamba CCM itatwaa kiti cha Kalenga Jumapili ijayo,” alisema Nape.

MANGULA AISHANGAA CHADEMA
Naye Mangula akimnadai mgombea wa CCM, Godfrey Mgimwa, kwenye vijiji vya Tosamaganga na Kalenga, wilaya ya Iringa Vijijini jana, alisema wamejipanga kulinda wapiga kura wake kwa kutumia vijana zaidi ya 260 ambao  wamesambazwa katika kata zote 13 za jimbo la Kalenga kwa uwiano wa  vijana 20 kila kata.

Alisema anawashangaa Chadema kwa  kupeleka idadi kubwa ya makada kutoka nje ya Kalenga, magari 75 na helikopta mbili kwa kisingizio cha kulinda kura wakati jukumu hilo ni la Jeshi la Polisi pamoja na mawakala wa vyama vya siasa ambao watakuwapo ndani ya vituo kwa ajili ya kila mmoja kuhakiki kura za mgombea wake.

 “Nawashangaa sana Chadema kwa kuleta makada 1,000 na magari 75 pamoja na helkopta mbili kwa kisingizio cha kulinda kura wakati kila kituo kitakuwa na mawakala wa kila chama kwa ajili ya kuhakiki kura zao,” alisema Mangula.

CHIFU KULINDA KURA ZA CHADEMA

Katika hatua nyingine, uchaguzi ambao umeugawa ukoo wa Chifu wa Kabila la Wahehe baada ya Naibu Chifu, Gerald Malangalila, kutangaza kukiunga mkono Chadema na kwamba  atakuwa mmoja wa mawakala watakaosimamia kura za mgombea wa chama hicho.

“Nimeanza mageuzi ya kifikra katika mikutano tisa niliyoifanya kwa helkopta jana, lakini pia nasema wazi wazi kwamba mimi ni mmoja wa mawakala wa Grace Tendega siku ya Machi 16. Ndugu zangu, kwa Wahehe, uchifu unarithiwa lakini ubunge haurithiwi...na kwa namna ya pekee, nimejitosa kulinda heshima yetu isivurugwe na mtu yeyote kwa sababu ya tamaa ya madaraka,” alisema Malangalila akimnadi mgombea huyo katika kijiji cha Mgama.

Februari 19, mwaka huu, wakati Chadema wanazindua rasmi kampeni zake katika jimbo la Kalenga, Chifu wa Kabila la Wahehe, Mtwa Mfuwimi wa II, Abdul Adam Sapi Mkwawa, alivitaka chama hicho na CCM kuendesha kampeni zao kistaarabu bila ya kuruhusu vurugu wala umwagaji damu.

 Wiki moja baadaye, akiwa katika uzinduzi wa kampeni za CCM, Chifu Abdul Mkwawa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Igwachanya, Kata ya Mseke, alisema anakiunga mkono chama hicho na kutoa baraka kwa mgombea wake, Mgimwa kuvaa viatu vya ubunge vya marehemu baba yake, Dk. William Mgimwa.

 Wakati huo huo; Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi Wilaya ya Iringa Vijijini, Bonus Kivawo, amejitosa pia kumnadi mgombea wa Chadema huku akiahidi pia kuwa mmoja wa mawakala wake katika Kijiji cha Magulilwa ambacho pia yeye ni Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho.

Uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge cha Kalenga unafanyika kujaza nafasi iliyoachwa na Marehemu Dk. Mgimwa, aliyefia hospitali ya Kloof Med- Clinic mjini Pretoria, Afrika Kusini Januari mosi mwaka huu


TASWIRA ZAIDI ZA KAMPENI ZA UBUNGE KALENGA

Meneja Kampeni wa Chama cha Deokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, Alphonse Mawazo, akicheza ngoma ya jamii ya kimasai baada ya kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba kumnadi mgombea ubunge wa chama hicho, Grace Tendega Mvanda, jana asubuhi. 


Mzee wa Mila wa Kimasai katika Kijiji cha Mfyome, Lioper Ilmuduji, akimpatia baraka mgombea ubunge  wa CHADEMA katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, Bi. Grace Tendega Mvanda, wakati chama hicho kilipofanya kampeni ya nyumba kwa nyuma kuomba kura kwa wananchi katika kijiji hicho jana asubuhi.

. Mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, Bi. Grace Tendega Mvanda akishiriki chakula cha kimila pamoja na watu wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Mfyome jana asubuhi baada ya msafara wa mgombea huyo kufika kijijini hapo kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba.

Mgombea Ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi mdogo Jimbo la Kalenga, Grace Tendega Mvanda, akizungumza kuomba kura wakati chama hicho kilipofanya kampeni ya nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu katika Kijiji cha Mfyome, jana asubuhi.


TASWIRA ZA KAMPENI YA UBUNGE KALENGA

Mgombea akipokelewa Lumuli

Heche akihutubia Lumuli;

Meneja wa Kampeni za mgombea ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Alphonce Mawazo, akimwelezea mtoto Zakina Miwela, anayesoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Lumuli, ambaye ni mtoto wa kiongozi wa CCM wa kijiji hicho, anavyoonekana bila viatu na sare zake kuchanika, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kijijini hapo jana.

Meneja wa Kampeni za mgombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Alphonce Mawazo na mgombea, GraceTendega, wakizungumza na akinamama wa kijiji cha Lumuli, katika kikao maalumu baada ya mkutano wa kampeni, zilizofanyika kijijini hapo jana.






No comments:

Post a Comment