Friday, March 21, 2014


Amos Wako aitahadharisha Tanzania kuhusu uundaji wa Katiba Mpya

By Beatrice Bandawe ;   21st March 2014

Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya ambaye sasa ni Mbunge wa Busia Mashariki nchini humo, Amos Wako, akihutubia wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana. Wako alikuwa akitoa uzoefu wa Kenya kwenye kuandika katiba mpya. Picha/Khalfan Said
Watanazania  wametahadharishwa kutoiga uzoefu wa mchakato wa kupata katiba mpya kutoka nchi nyingine za Kiafrika ikiwamo Kenya kwa kuwa mchakato huo sio Biblia.

Seneta Amos Wako, Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa serikali ya Kenya, aidha, alisema sababu nyingine ni kila nchi kuwa na mazingira yake.

Akitoa mada kwenye semina ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba jana mjini hapa, Seneta Wako alisema mifumo ya upataji katiba unatofautiana kati ya nchi na nchi.

“Natoa tahadhari, msiige uzoefu kutoka nchi nyingine, inaweza kuwa isiwe na faida kwenu, hii siyo Biblia," alisema.

Alisema  katiba yao ina mfumo wa  mgawanyo wa madaraka kwa sababu wakati inaundwa Wakenya wengi waliona madaraka mengi yanapaswa kwenda kwa wananchi na kwamba baada ya kupatika kwa katiba hiyo, iliundwa Tume ya kusimamia utekelezaji wa Katiba.

Seneta Wako aliyeshika wadhifa huo katika awamu mbili za uongozi za Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki, alisema tume hiyo ni huru ambayo inafuatilia utekelezaji wa katiba na kutoa ushauri kwa serikali.

Alieleza kuwa eneo ambalo Tume hiyo ilifanikiwa ni siku ambayo Rais wa Kenya  alipowateua Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu kwa siku moja na ilisema ni kinyume na katiba na bunge lilisema ni kinyume na katiba na kuwa uamuzi ulitenguliwa.

Aidha, alisema waliona hakuna mfumo mzuri wa mgawanyo wa rasilimali na mgawanyo wa bajeti mahali ilipo serikali au kuliko na wananchi wengi ambako hakuna maendeleo kuwe na umuhimu wa pekee katika katiba.

Pia, alisema Katiba ya Kenya ina mfumo wa majimbo 47 ya utawala na kuwa wakati Kenya inapata uhuru kulikuwa na wilaya 42 na kuwa  inaonekana  huo utakuwa mwanzo mzuri.

Alitoa mfano kwamba jimbo lake la Busia ambalo lina wabunge saba, majimbo mengi ya Kenya yana wajumbe watano na maeneo katika Jiji la Nairobi yana wabunge 16.

Alisema kila jimbo kuna seneta mmoja na vile vile kuna Gavana ambaye ni kama afisa mtendaji mkuu wa eneo na ana kamati ya watendaji inayomzunguka katika kutekeleza majukumu.

Alisema baada ya kupitishwa kwa Katiba ya Kenya kwenye mikutano ya hadhara magavana hao wanaonekana kama marais wa maeneo wanayotoka na wajumbe wa kamati ya utendaji wanajiita mawaziri katika maeneo husika.

Seneta Wako alisema mfumo huo wa mgawanyo wa madaraka ni wa pekee na unatumika Kenya na kwamba huenda usifanye kazi sehemu nyingine.

Alisema walioamua kufanya hivyo ili kupata maendeleo ya haraka na kwamba umepata mafanikio kutokana na hivi sasa halmashauri nyingi kujiendesha zenyewe.

Kadhalika, Seneta Wako alisema kuwa katiba mpya ya Kenya imempunguzia Rais madaraka ya uteuzi kutokana na maofisa waandamizi kuomba kazi hizo.

Kwa mfano, alisema kuwa nafasi za Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mawaziri hawateuliwi na rais moja kwa moja, bali nafasi zao hutangazwa na baadaye hufanyiwa usaili kupitia televisheni na baadaye walioshinda kuthibitishwa na Bunge.

Akiuliza swali kuhusu uzoefu huo, Mjumbe Profesa Abdallah Safari alisema, ibara  8-178 ya Katiba ya Kenya, inasema Kiswahili ndio lugha ya taifa ya Kenya, lakini katika mikutano ya hadhara na hata elimu nchini humo inatolewa kwa Kiingereza na mfano mzuri ni yeye (Wako) kutoa mada yake kwa Kiingereza jana, hivyo anatoa ushauri gani kuhusiana na namna ya kukienzi Kiswahili?

Mjumbe mwingine, Dk. Nancy Mrikaria alitaka kujua kwa nini michakato ya katiba inayofanyika katika nchi za kiafrika kunatokea matatizo ya watu kupoteza maisha na wengine kuishia jela.

Naye Job Ndugai alitaka kujua Wako anachukuliaje  akiwa mshiriki mkuu wa kuandika rasimu ya  katiba ya Kenya na ilipopelekwa kwa wananchi ilishindwa?

Akijibu hoja hizo, Seneta Wako alisema Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Kenya, lakini kutokana na Wakenya wengi kutoizungumza vizuri, wanaendelea kujifunza.

Hata hivyo, alisema kwa sasa Wakenya wengi wanajitahidi kuzungumza lugha hiyo.

Kuhusu rasimu ya kwanza kutokubaliwa, Seneta Wako alisema hali hiyo ilitokana na mchakato wake kushirikisha wajumbe wengi wa chama tawala bila kushirikisha vyama na taasisi zingine.

Akizungumzia vurugu, alisema alisema hali hiyo inatokana na  mchakato huo kuwa jambo jipya, ambalo  siyo rahisi kukubalika kwa urahisi.
 
SOURCE: NIPASHE 

Amos Wako: Msipuuze maoni ya wananchi

Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali ya Kenya, Seneta Amos Wako akizungumza jana, wakati wa Semina ya Bunge Maalumu la Katiba. Picha na Salim Shao 
Na Habel Chidawali na Editha Majura, Mwananchi
  • Awataka Wajumbe wa Bunge la Katiba watunge Katiba inayotokana na maoni na matakwa ya wananchi ili kuepusha migogoro.

Dodoma. Mwanasheria Mkuu (AG) mstaafu wa Kenya, Amos Wako amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutokupuuza maoni ya wananchi katika kutunga Katiba ya nchi vinginevyo watazua mgogoro.
Wako, ambaye kwa sasa ni Seneta wa Busia ya Mashariki nchini Kenya, alitoa ushauri huo jana katika semina kwa wajumbe wa Bunge la Katiba kuhusu uzoefu wa namna nchi hiyo ilivyopitia misukosuko ya kuipata Katiba mpya.
Wako ambaye kwa miaka 21 alikuwa katika wadhifa wa AG, alisema matukio mengi yaliyosababisha Kenya kutokupata Katiba yao kwa wakati, yalitokana na kutokuwashirikisha wananchi moja kwa moja katika mchakato.
Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa 2: 11, mwanasheria huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba ya Kenya alionya pia kuwa Katiba inayotengenezwa hapa nchini isiwe ya kunukuu kutoka katika mataifa mengine kwa sababu mahitaji yanatofautiana kwa kila nchi.
“Katiba isiwe ya mazungumzo kutoka kwa viongozi pale Dar es Salaam, kwani itakuwa ni mali ya watu wachache na ambayo lazima itapingwa, hata sisi tulianza hivyo lakini tulishindwa vibaya,” alionya Wako.
Aliimwagia sifa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni Jumanne iliyopita, kwamba kwa mtindo ilivyowasilishwa inaonekana kuwajali na kuwapa nafasi zaidi wananchi wa hali ya chini.
“Pamoja na hayo, lakini Katiba hii ikiingiliwa zaidi na kutekwa na wanasiasa au kikundi cha watu wachache kwa masilahi yao, inaweza kuharibika kama ilivyotokea kwetu Kenya ambako Kanu walikuwa wakipinga kila kitu wakatufanya tuingie katika mgogoro.”
Alisema kuwa mitazamo ya wanasiasa huwa ni tatizo na hatari katika kutafuta Katiba mpya na dawa pekee na ya maana ni kutoa nafasi kwa wananchi waamue wenyewe.
“Mfumo uliowekwa katika mchakato wa kuunda Katiba mpya nchini kwenu, kwamba Rasimu ya mwisho ya Katiba itoke bungeni na kupelekwa moja kwa moja kwa wananchi ni mzuri, ni muhimu maoni ya wananchi ya awali yazingatiwe,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Bunge Maalumu limeaminika kufanya kazi hiyo ili kuwasaidia wananchi kufikia malengo yao.
Uzoefu wa Kenya
Akizungumzia uzoefu wa Kenya katika kupata Katiba mpya alisema walianza kwa kukabiliana na changamoto kubwa ya ukabila ambayo kila jamii ilikuwa haiamini kundi jingine katika kutafuta usawa, jambo alilosema ni tofauti na Tanzania.
 
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment