Wednesday, March 19, 2014

JAJI WARIOBA AWASILISHA RASIMU YA PILI YA KATIBA MPYA BUNGE MAALUM LA KATIBA,March 18, 2014



JAJI WARIOBA ASEMA ILI KUUFANYA MUUNGANO UWE IMARA TUNAHITAJI SERIKALI TATU

PG4A2542

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba akiwasilisha Rasimu ya Katiba  mpya mbele ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, bungeni mjini Dodoma Machi 18, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Warioba akata ngebe za CCM

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amezima rasmi sakata la makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulazimisha Bunge Maalumu la Katiba kukataa pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Akiwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba bungeni jana, Jaji Warioba alisema uchambuzi uliofanywa na tume yake umezingatia maoni ya wananchi, historia  na hali halisi, na kwamba ili muungano udumu serikali tatu hazikwepeki.
Alisema tume ilitafakari maoni mbalimbali yaliyotolewa na wananachi na makundi, na ilirejea ripoti kadhaa za miaka zaidi ya 20 mfululizo, ikazingatia malalamiko ya Zanzibar na Tanganyika, mgongano wa kikatiba kati ya Katiba ya Zanzibar na ya Muungano, na mengine mengi.

 PG4A2567

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimpongeza Mwenyekiti wa Tume ya  Mabmadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba (kushoto) baada ya Mwenyekiti huyo kuwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya bele ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba Bungeni Mjini Dodoma Machi 18, 2014.Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Bunge  Maalum la Katiba, Samia Suluhu (kuli), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, Profesa  Anna Tibaijuka,  Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (watatu kushoto) na  watatu kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani  , Mathias Chikawe. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
 
Shivji na Mtizamo wa Muundo wa Serikali
Mwandishi Wetu
Raia  Mwema .Toleo la 300 , 26 Jun 2013
WAKATI Profesa Issa Shivji akihoji asili ya wazo la serikali tatu katika rasimu ya katiba mpya ambayo imejenga uhalali wake kutokana na hati ya Muungano ya mwaka 1964 inayotaka serikali mbili, Jaji Joseph Warioba, amewatolea uvivu wakosoaji wa rasimu hiyo, Raia Mwema linaripoti.
Katika mazungumzo yake na mwandishi wetu, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya, Warioba ameelezea kufurahishwa zaidi na ukosoaji wanaopendekeza pia mbadala wa kile wanachokikosoa kutoka katika rasimu hiyo ambayo itajadiliwa kwa kina katika mabaraza ya katiba hivi karibuni.
“Tumetoa rasimu, tunataka mawazo ya watu kwa sababu tulipokwenda kwao tulichukua maoni ambayo pengine katika rasimu hii hayapo au yapo kwa sababu tulichambua na kuchagua maoni hayo. Watoe maoni yao kwa uhuru, lakini si kukosoa tu pekee, bali wakosoe na kupendekeza. Ukikosoa pekee haitusaidii sana.
“Lakini hadi sasa katika hatua hizi za awali mara baada ya kutolewa rasimu, tunaridhika na mchakato na kwa kweli ndicho tulichotarajia, ukosoaji na maoni mengine mbadala,” alisema Warioba.
Mtazamo huo wa Warioba unajitokeza ikiwa ni takriban wiki moja tangu Profesa Issa Shivji, ambaye ni gwiji wa masuala ya katiba na sheria, awasilishe mada juu ya rasimu hiyo katika kongamano la Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Juni 21, mwaka huu, katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kati ya ukosoaji aliofanya Profesa Shivji ni pamoja na kuhoji uhalali wa mapendekezo ya serikali tatu, katika rasimu ambayo inajieleza kujenga nguvu zake kutokana na hati ya Muungano wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar, ya mwaka 1964.
Katika mada yake ambayo imeanza kuchapishwa na gazeti hili kwa awamu, Shivji anasema hati ya makubaliano ya 1964 ni msingi wa rasimu ya katiba na katiba hiyo ni mwendelezo wa makubaliano hayo.
“Ukiangalia kwa jicho la kisheria, ukisema Hati ndio msingi, maana yake ni kwamba Hati bado inaendelea kuwa na nguvu ya kisheria na ndiyo sheria kuu inayotawala Katiba. Lakini Hati iliweka serikali mbili; sasa, iweje rasimu inayozungumzia serikali tatu iwe na msingi ambao ulijengeka kwenye serikali mbili?
“Katiba iliyojikita kwenye serikali tatu haiwezi, kwa vyovyote vile, ikawa mwendelezo wa Hati. Ni kweli kabisa kwamba Hati ya Makubaliano ya 1964 ni chanzo cha Muungano. Historia hii, kama inavyostahili, imewekwa kwenye Utangulizi (wa rasimu). Lakini masharti ya katiba yenye nguvu za kisheria hayawezi tena kurudia historia.
“Ukitaja maneno kama haya katika masharti ya Katiba, kimahakama inachukuliwa kwamba nia yako ilikuwa kuipa Hati nguvu ya kisheria. Nina uhakika kabisa kwamba haikuwa nia ya Tume kuifufua Hati ya 1964 na kuipa nguvu ya kisheria.
Pia, ninaamini kabisa kwamba Tume iliyosheheni wanasheria wazoefu na waliobobea huenda walijua na kuelewa kabisa walichokuwa wanaandika.
“Kwa hivyo, haiwezekani kwamba walikosea, au kuteleza, bali ilikuwa ‘kusalimu amri’ na “kuelewana” ili mambo yaendelee. Ndivyo tulivyopata ibara legelege ambayo kisheria haina kichwa wala mkia,” anasema Shivji.
Ingawa Shivji hakutaja kwa majina watalaamu wenzake wa sheria walioko katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini ni dhahiri alikuwa akiwazungumzia Profesa Palamagamba Kabudi, Dk. Sengodo Mvungi, Said El Maamry na wengine.
Hata hivyo, wakati Shivji akihoji uhalali wa rasimu ya Katiba kupendekeza serikali tatu kinyume cha Hati ya Makubaliano, habari za uhakika zinaeleza kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kipo katika mvutano wa ama kuweka wazi msimamo wake kuhusu idadi ya serikali zinazotajwa kwenye rasimu ya Katiba ama kuwaachia kwanza wanachama wake kuamua kwenye mabaraza ya Katiba.
Kutokana na mvutano huo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameitisha ‘kimyakimya’ Kamati Kuu ya chama hicho ili kufikia uamuzi wa pamoja wa ama kuweka wazi msimamo wake wa idadi ya serikali ndani ya rasimu ya Katiba ama la.
Gazeti hili limetaarifiwa kwamba sehemu kubwa ya wanachama wa chama hicho wanashinikiza chama chao kuweka msimamo na kutamka wazi kinaunga mkono serikali mbili, na si tatu, tofauti na vyama vingine, kikiwamo Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Lakini msomi mashuhuri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo, naye amekosoa rasimu ya Katiba mpya akisema imeshindwa kuwabeba vijana, akirejea suala la ukomo wa umri katika kugombea nafasi za urais na hata ubunge na maelezo yake hayo yamechapishwa kwa kirefu katika gazeti hili.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba mara kadhaa, baada ya kuzinduliwa kwa rasimu ya Katiba, alikaririwa akiunga mkono rasimu hiyo kwa kiwango kikubwa.
Ingawa rasimu hiyo ya Katiba mpya imependekeza masuala mbalimbali mapya katika utawala nchini, lakini mjadala mkali umekuwa ukijikita zaidi katika idadi ya serikali, wengine wakiunga mkono serikali tatu kama ilivyopendekezwa na wengine wakipinga.











No comments:

Post a Comment